Mason Greenwood kimenuka tena

Muktasari:
- Mchezaji huyu wa zamani wa Man United ameonyesha kiwango cha kuvutia tangu kuanza kwa msimu huu, akifunga magoli 15 katika mechi 24 na kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa Ligue 1.
MARSEILLE, UFARANSA: WAKATI mambo yakionekana kumnyookea baada ya kupitia kipindi kigumu akiwa na Manchester United, mapya yaibuka tena kwa mshambuliaji wa Olympique Marseille, Mason Greenwood baada ya kutoanzishwa katika mchezo wa wikiendi iliyopita dhidi ya Lens ambapo kocha wake Roberto De Zerbi alisema hakumwanzisha kwa sababu haridhishwi na utendaji kazi wake.
Mchezaji huyu wa zamani wa Man United ameonyesha kiwango cha kuvutia tangu kuanza kwa msimu huu, akifunga magoli 15 katika mechi 24 na kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa Ligue 1.
Hata hivyo, kwa mujibu wa De Zerbi staa huyu anakosa ufanisi linapokuja suala la kuisaidia timu kukaba pale inapopoteza mpira.
Licha ya kufunga mabao matatu katika mechi zake tano zilizopita, hiyo haikumzuia De Zerbi kumweka nje katika mechi hiyo dhidi ya Lens.
"Nilimhitaji hapa, nilikuwa nikisema mara kwa mara, alikuwa mchezaji wa kwanza niliyekuwa nakiwasiliana naye, hata kabla sijajiunga na Marseille. Nilikuwa tayari nimeshaongea na baba yake. Hakuna mtu anayeweza kumheshimu zaidi kuliko mimi."
"Lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba natarajia zaidi kutoka kwake. Anapaswa kufanya zaidi, kwa sababu kile anachoonyesha kwa sasa hakitoshi."
"Ikiwa anataka kufikia lengo lake la kuwa mchezaji bora, lazima awe na usahihi, kutoa zaidi na kuwa na shauku awapo uwanjani, vinginevyo, sisi kama timu kila wakati tutakuwa tunaanguka kwenye mtindo uleule, tunacheza vizuri sana, kisha tunafungwa kama ilivyokuwa dhidi ya Auxerre, tumekuwa na mawimbi katika matokeo yetu na hiyo ni kitu sitaki."
Greenwood aliingia akitokea benchi katika mchezo huo dhidi ya Lens, lakini Marseille ilipoteza kwa bao la dakika za jioni lililofungwa na Neil El Aynaoui.
Baada ya kuonekana kama mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa katika kikosi cha Man United, aliondoka kwenye timu hiyo msimu uliopita baada ya kukamatwa Januari 2022 kwa kosa la unyanyasaji wa kijinsia lakini baadae hakukutwa na hatia lakini hakurejea Man United badala yake alitolewa kwa mkopo kwenda Getafe msimu uliopita na akafunga mabao 10 na kutoa asisti sita na mwisho wa msimu akauzwa kwenda Marseille aliyoanza kuitumikia msimu huu.