Masharti ya Mourinho yakubaliwa Real Madrid
Muktasari:
- Katika makubaliano hayo, kocha huyo raia wa Ureno amepewa mamlaka makubwa na ya kipekee ambayo yatamwezesha kuendesha timu hiyo kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu yeyote.
REAL Madrid imeripotiwa kukubali masharti yote magumu ya kocha José Mourinho ili kufanikisha safari yake ya kurejea klabuni hapo.
Katika makubaliano hayo, kocha huyo raia wa Ureno amepewa mamlaka makubwa na ya kipekee ambayo yatamwezesha kuendesha timu hiyo kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu yeyote.
Sharti la kwanza na kubwa zaidi ambalo uongozi wa Real Madrid umeliridhia ni kumpa Mourinho udhibiti kamili wa masuala ya usajili wa wachezaji wapya pamoja na uamuzi wa nafasi zao uwanjani.
Aidha, klabu hiyo imekubali kuwa wajumbe wa bodi hawatakuwa na ruhusa ya kuingilia kati au kuhudhuria vipindi vya mazoezi ya timu hiyo, jambo linalompa kocha huyo utulivu wa kutengeneza mbinu zake.
Mbali na masuala ya uwanjani, Mourinho ameweka msimamo mkali kuhusu uhusiano wake na vyombo vya habari kwa kukataa kushiriki mikutano ya waandishi wa habari isiyo na tija au maana yoyote kwake.
Hatua ya mwisho iliyobarikiwa na miamba hiyo ya Hispania ni ruhusa ya Mourinho kuja na benchi lake zima la ufundi atalolichagua, akiondoa wasaidizi waliopo sasa.
Mourinho ambaye kwa sasa ni kocha wa Benfica ya Ureno akiwa na mkataba nayo hadi Juni 30, 2027, anahusishwa kurejea Real Madrid, klabu aliyoifundisha kuanzia Julai 2010 hadi Juni 30, 2013, akishinda mataji matatu katika mechi 178 alizosimamia ambayo ni Copa del Rey (2010-2011), La Liga (2011-2012) na Spanish Super Cup (2012-2013).
Mabosi wa Real Madrid wanataka kumrejesha Mourinho kikosini hapo kuchukua nafasi ya Álvaro Arbeloa.