Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mourinho kutua Madrid wiki ijayo

Muktasari:

  • Kocha huyo raia wa Ureno anatarajiwa kutangazwa rasmi ndani ya siku chache zijazo huku akipewa ofa ya mkataba wa awali wa miaka miwili kuchukua nafasi ya Alvaro Arbeloa ambaye yupo kwenye presha kubwa kufuatia mwenendo mbaya wa Real Madrid

MADRID, HISPANIA: JOSE MOURINHO yupo mbioni kurejea tena kuinoa Real Madrid kwa mara ya pili baada ya ripoti kutoka Hispania na Ureno kudai kuwa makubaliano tayari yamekamilika kati yake na mabosi wa klabu hiyo wakiongozwa na rais Florentino Perez.

Kocha huyo raia wa Ureno anatarajiwa kutangazwa rasmi ndani ya siku chache zijazo huku akipewa ofa ya mkataba wa awali wa miaka miwili kuchukua nafasi ya Alvaro Arbeloa ambaye yupo kwenye presha kubwa kufuatia mwenendo mbaya wa Real Madrid

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Hispania, Mourinho aliwashinda makocha wengine waliokuwa kwenye hesabu za kupewa kazi hiyo akiwemo Didier Deschamps na Mauricio Pochettino huku Perez akiamini kuwa uzoefu na ukali wa Mourinho vinaweza kurejesha nidhamu ndani ya kikosi hicho kilichokumbwa na migogoro ya ndani.

Mourinho mwenye miaka 63 anatarajiwa kuiongoza Benfica kwa mara ya mwisho leo, Jumamosi dhidi ya Estoril kabla ya kuondoka rasmi. Ingawa amekanusha kuwa na mawasiliano na Madrid, amekiri kuwa wiki ijayo itakuwa muhimu kwa ajili ya hatma yake.

“Nazungumza na rais wa Benfica karibu kila siku lakini kuhusu Real Madrid sijafanya mawasiliano yoyote. Wiki ijayo itakuwa muhimu kwa maisha yangu ya baadaye na pia Benfica,” alisema Mourinho.

Ripoti zimeeleza kuwa ndani ya mkataba wake na Benfica kuna kipengele kinachoiruhusu Madrid kulipa kiasi cha pauni 2.6 milioni kama fidia ili kumchukua kocha huyo ndani ya siku 10 baada ya mechi ya mwisho ya msimu.

Mourinho aliwahi kuifundisha Madrid kati ya 2010 hadi 2013 na kutwaa taji la LaLiga, Copa del Rey pamoja na Spanish Super Cup huku akijenga ushindani mkubwa dhidi ya Barcelona iliyokuwa chini ya Pep Guardiola.

Urejeo wake unatajwa kuchochewa pia na hali ya sintofahamu ndani ya kikosi cha Madrid baada ya kuwepo kwa taarifa za migogoro kati ya baadhi ya nyota wa timu hiyo akiwemo Federico Valverde, Aurelien Tchouameni na Antonio Rudiger.

Pia mshambuliaji nyota Kylian Mbappe alizua mjadala baada ya kudai kuwa amewekwa kama mshambuliaji wa nne kwenye mipango ya timu hiyo, jambo lililoonyesha wazi kuwepo kwa migawanyiko ndani ya klabu hiyo.