Arbeloa amfagilia njia Mourinho
Muktasari:
- Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kuelekea mchezo wa leo, Jumapili dhidi ya Sevilla FC, Arbeloa alizungumzia pia hali ya ndani ya kikosi, hatma yake kama kocha na mvutano unaoendelea kuhusu nyota wa timu hiyo, Kylian Mbappe.
MADRID, HISPANIA: KOCHA wa muda wa Real Madrid CF, Alvaro Arbeloa amezua mjadala mpya baada ya kusema wazi kuwa kwa mtazamo wake kama 'Madridista' kocha bora zaidi katika historia ya klabu hiyo ni José Mourinho.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kuelekea mchezo wa leo, Jumapili dhidi ya Sevilla FC, Arbeloa alizungumzia pia hali ya ndani ya kikosi, hatma yake kama kocha na mvutano unaoendelea kuhusu nyota wa timu hiyo, Kylian Mbappe.
Arbeloa alisema hana shaka na nafasi ya Mourinho katika historia ya klabu hiyo, akisisitiza kuwa kocha huyo wa Ureno “ni namba moja” kwa mchango wake na falsafa yake ya ushindi.
“Kwa upande wangu kama Madridista, Mourinho ni namba moja. Niliamini hivyo mwezi uliopita na bado naamini hivyo. Yeye ni mmoja wetu na atabaki hivyo daima,” alisema Arbeloa.
Kauli hiyo imezua mjadala mkali ndani na nje ya Hispania huku wachambuzi wakiiunganisha na presha inayoendelea kwa uongozi wa Real Madrid kutokana na matokeo yasiyoridhisha msimu huu.
Licha ya mvutano huo wa kauli wakati ambao Mourinho atajwa kuwa mbioni kurejea Real Madrid, Arbeloa alijikita zaidi kueleza maandalizi ya mchezo dhidi ya Sevilla, akitaja kuwa ni moja ya mechi ngumu zaidi kutokana na kiwango cha wapinzani wake.
Alisema Sevilla wameonyesha maboresho makubwa chini ya uongozi mpya na wamekuwa na mfululizo mzuri wa matokeo katika michezo yao ya hivi karibuni.
Arbeloa pia alilazimika kugusia sakata linalomhusu Mbappe ambaye amekuwa kitovu cha mijadala baada ya ripoti za kutoridhishwa na nafasi yake kikosini na mzozo wa ndani.
Kocha huyo alisema kuwa hana mgogoro binafsi na mshambuliaji huyo wa Kifaransa, akieleza kuwa mazungumzo yao yamekuwa ya kawaida na yenye lengo la kudumisha utulivu wa kikosi.
“Nilimwona na nikamwambia atulie, kwamba nitashughulikia kila kitu. Tumeshaongelea mambo haya kabla ya mchezo na hakuna tatizo,” alisema.
Aliongeza kuwa hisia za Mbappe kutoridhishwa ni jambo la kawaida kwa mchezaji mkubwa, hasa pale anapokosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.