Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mashabiki wataka tiketi Kombe la Dunia 2026 zisiuzwe tena

KOMBE LA DUNIA Pict

Muktasari:

  • Shirika la Football Supporters Europe (FSE) limeishambulia vikali FIFA na kuelezea gharama hizo ni kama usaliti mkubwa kwa mashabiki wa mpira wa miguu.

NEW YORK, MAREKANI: MASHABIKI wa soka wenye hasira wametaka uuzaji wa tiketi za Kombe la Dunia 2026 usitishwe mara moja kutokana na bei za kinyonyaji.

Shirika la Football Supporters Europe (FSE) limeishambulia vikali FIFA na kuelezea gharama hizo ni kama usaliti mkubwa kwa mashabiki wa mpira wa miguu.

FSE ilionyesha takwimu zinazoonyesha kuwa bei za tiketi zimepanda kwa asilimia 370 ikilinganishwa na Kombe la Dunia la 2022 lililofanyika Qatar.

Takwimu hizo zinaonyesha pia kuwa shabiki anayepanga kufuatilia timu yake ya taifa katika mashindano yote yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico atalazimika kutumia walau Pauni 5,141.8, ikilinganishwa na Pauni 1,095.4 miaka minne iliyopita.

Kiasi hicho hakijumuishi gharama za usafiri, wala malazi na chakula ambavyo kwa sasa vimepanda bei nchini Marekani.

Katika taarifa yao FSE ilieleza: “Football Supporters Europe imeshtushwa na bei za tiketi za kiunyonyaji zilizowekwa na FIFA kwa mashabiki wanaohitaji kutazama Kombe la Dunia mwakani. Kutokana na taarifa tulizonazo kwa sasa, ikiwa shabiki atahitaji kutazama  mechi zote za timu yake kuanzia makundi hadi fainali, atalazimika kulipa walau Dola 6,900, karibu mara tano zaidi ya Kombe la Dunia la FIFA 2022 nchini Qatar. Mashabiki wa timu za taifa wanatarajiwa kulipa kiasi hiki chote mapema mwaka 2026 ili kupata nafasi ya kufuatilia timu zao hadi fainali.”

“Huu ni usaliti mkubwa wa utamaduni wa Kombe la Dunia, unaopuuzia mchango wa mashabiki katika kufanya mashindano haya yawe ya kuvutia.”

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia, hakutakuwa na bei moja thabiti kwa mechi zote za hatua ya makundi. Badala yake, FIFA inaangalia kulingana na vigezo visivyoeleweka kama mvuto wa mechi husika.”

Mashabiki watalazimika kulipa jumla ya Pauni 436 ili kutazama mechi tatu za hatua yote ya makundi, kiasi ambacho ni kikubwa sana ikilinganishwa na Pauni 154 kilichokuwa kinalipwa Qatar, ambapo tiketi ya mechi moja ya raundi ya kwanza ilikuwa Pauni 51.4 tu.

Mbali ya makundi, raundi inayofuata ya 32 bora inatarajiwa kugharimu mashabiki Pauni 175.1 na baada ya hapo mashabiki watalazimika kulipa Pauni 219.8 kutazama mechi ya Raundi ya 16, Pauni 506.7 kwa robo fainali na Pauni 685.6 kwa nusu fainali, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka Pauni 71.5, Pauni 153.5 na Pauni 266 kwa michuano ya Qatar na Russia.

Vilevile katika mechi ya fainali, mashabiki watalazimika kulipa Pauni 3,118.6 ili kununua tiketi, ambayo ni ongezeko  la asilimia 593 ikilinganishwa na bei ya Pauni 450.1 iliyokuwa inauzwa tiketi ya fainali huko Qatar.