Mashabiki Real Madrid washangaa Bellingham kutoonekana kwenye kalenda ya 2026
Muktasari:
- Klabu hiyo ya kihistoria ya Hispania, imefikia uamuzi huo ikiwa ni siku chache baada ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel kumtema Bellingham kwenye kikosi chake kwa ajili michezo ya kimataifa ya kalenda ya FIFA.
Uongozi wa Real Madrid umezua maswali kwa baadhi kwa mashabiki wa klabu hiyo kufuatia kumuondoa Jude Bellingham katika kalenda ya klabu hiyo mwaka 2026, wakihoji mustakabali wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22.
Klabu hiyo ya kihistoria ya Hispania, imefikia uamuzi huo ikiwa ni siku chache baada ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel kumtema Bellingham kwenye kikosi chake kwa ajili michezo ya kimataifa ya kalenda ya FIFA.
Mwaka 2025, Bellingham alionekana kwa ukubwa kwenye jalada la mbele la kalenda ya Real Madrid ya mwaka 2025 na alipewa nafasi ya mwezi Agosti. Lakini kwenye toleo jipya la kalenda ya mwaka 2026, linalouzwa kwa Pauni 10.99, hajaonekana kabisa.
Wengine ambao picha zao hazimo kwenye toleo la kalenda ya mwaka 2026 ni Trent Alexander-Arnold, ambaye alijiunga na Real Madrid kutoka Liverpool kwa Pauni 8.7 milioni, mwanzoni mwa msimu huu 2025-2026, baada ya mkataba wake kumalizika.
Wachezaji waliopata nafasi kwenye jalada la mbele ni pamoja na Dean Huijsen, beki aliyesajiliwa kwa Pauni 50 milioni kutoka Bournemouth, na nyota kinda kutoka Uturuki mwenye umri wa miaka 20, Arda Guler.
Ndani ya kurasa za kalenda, majina yaliyopata nafasi ni pamoja na wachezaji wa muda mrefu kama Dani Carvajal (miaka 33) na Eder Militao (miaka 27).
Bellingham, mzaliwa wa Birmingham, ameanza kupoteza nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid, baada ya kurejea kutoka kwenye jeraha la bega mwezi Septemba.
Kocha wa England, Thomas Tuchel, amesema: "Bellingham amekosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha Real Madrid, hivyo nimeamua kumuacha kwenye kikosi changi kwa sasa.”
Nyota huyo wa zamani wa Borussia Dortmund, ameanza mechi moja ya Real Madrid tangu aliporejee kutoka kwenye jeraha mwezi Septemba.
Kocha Xabi Alonso alimpa nafasi ya kuanza katika kipigo cha kushangaza cha 5-2 dhidi ya Atletico Madrid, lakini kwenye mechi mbili zilizofuata, aliingia kama mchezaji wa akiba.
Alonso alisema kabla ya mechi dhidi ya Atletico kwamba anahitaji mchango wa Bellingham.
“Ninahitaji uwezo wake wa kubadilika uwanjani. Wachezaji wengine wana sifa tofauti na Bellingham," amesema Alonso.