Mashabiki Manchester City wamtabiria mabaya Arne Slot
Muktasari:
- Mechi 11 ilizocheza Liverpool kwenye Ligi Kuu England, imeshinda sita na kupoteza tano, huku ikiwa haijatoka sare yoyote msimu huu huku ikiwa imekusanya pointi 18.
LIVERPOOL, ENGLAND: “UTAFUKUZWA kazi mapema asubuhi,” waliimba mashabiki wa Manchester City kumlenga kocha wa Liverpool, Arne Slot kutokana na mambo yanavyokwenda kombo kwenye kibarua chake cha kuinoa miamba hiyo ya Anfield.
Slot ameshuhudia timu yake ikipoteza mechi tano kati ya sita ilizocheza hivi karibuni kwenye Ligi Kuu England na hivyo Liverpool kushuka hadi nafasi ya nane kwenye msimamo kutokana na kuwa na wastani mdogo wa tofauti za mabao. Na hapo bila ya kulizungumzia pengo la pointi nane walizoachwa na vinara Arsenal wakati ligi hiyo ikiwa imeingia kwenye mchezo wake wa 11.
Kiungo wa zamani wa Ligi Kuu England, Roy Keane, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka, alilielezea hilo linaloendelea kutokea Liverpool kuwa ni janga.
Keane amesema: “Kupoteza mechi saba kati ya 10 na kupoteza tano kwenye ligi hadi ligi ilipofikia kwa sasa, hilo ni janga kwa klabu kama Liverpool. Liverpool imekuwa timu dhaifu sana.”
Nani alitarajia hili? Kocha huyo Mdachi, Slot alifungulia pochi kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kufanya usajili wa kuboresha zaidi kikosi chake baada ya kubeba taji la Ligi Kuu England msimu uliopita, ambao ulikuwa msimu wake wa kwanza huko Anfield.
Lakini, wamiliki wa timu hiyo, FSG bila shaka kwa sasa wapo kwenye mshangao mkubwa kutokana na uwekezaji wao wa zaidi ya Pauni 426 milioni waliofanya kwenye dirisha lililopita ukishindwa kuleta mambo ya maana uwanjani.
Achana na lililowahi kuwakuta Jose Mourinho na Claudio Ranieri kufutwa kazi miezi michache baada ya kubeba ubingwa wa ligi. Hilo linaweza kutokea kwa Slot pia, endapo kama atashindwa kurekebisha mambo kwa haraka kwenye kikosi chake cha Liverpool.
Shida kubwa inayoonekana kuikabili Liverpool kwa sasa ni udhaifu kwenye safu ya ulinzi. Pengine kitendo cha kumkosa Marc Guehi kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili litakuwa ni pigo kubwa sana. Slot hakuweka mkazo kwenye usajili wa beki badala yake alitumia karibuni Pauni nusu bilioni kuboresha kwenye maeneo mengine.
Beki Mfaransa, Ibrahima Konate amekuwa na wakati mbaya msimu huu, huku pacha yake na Virgil van Dijk ikishindwa kumpatia Slot kitu ambacho anakihitaji. Umri wa Van Dijk, 34, umekwenda pia, hivyo nguvu imeanza kumtupa mkono.
Wakati Liverpool inatoa pesa nyingi kuboresha safu ya ushambuliaji ilipowanasa wakali kama Florian Wirtz, Alexander Isak na Hugo Ekitike iliamini kwamba wao watakachofanya ni kufunga mabao mara nyingi bila ya kujali mpinzani atafanya nini. Lakini, si Wirtz, Isak wala Ekitike, anayeweza kulifanya hilo kwenye mechi za Liverpool zilizochezwa hadi sasa hivyo, huku safu yao ya mabeki ikiwa imechoka na kuruhusu mabao kirahisi. Jambo hilo limeifanya Liverpool kuwa kwenye wakati mgumu kukabiliana na presha ya wapinzani kwenye mechi mbalimbali.
Kwenye Ligi Kuu England peke yake, Liverpool imeruhusu nyavu zake kuguswa mara 17 katika mechi 11, huku ikiwa imefunga mabao 18 tu, hivyo ina wastani wa bao +1 wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kwenye mikikimikiki ya ligi hiyo.
Mechi 11 ilizocheza Liverpool kwenye Ligi Kuu England, imeshinda sita na kupoteza tano, huku ikiwa haijatoka sare yoyote msimu huu huku ikiwa imekusanya pointi 18.
MECHI ZIJAZO ZA LIVERPOOL KWENYE EPL
Novemba 22 vs Nottm Forest (nyumbani)
Novemba 30 vs West Ham (ugenini)
Desemba 3 vs Sunderland (nyumbani)
Desemba 6 vs Leeds United (ugenini)
Desemba 13 vs Brighton (nyumbani)
Desemba 20 vs Tottenham (ugenini)
Desemba 27 vs Wolves (nyumbani)