Maresca anataka wazee Chelsea
Muktasari:
- Newcastle ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 katika kipindi cha kwanza kabla ya Chelsea kusawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Reece James na Joao Pedro.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amesema Chelsea ingeweza kunufaika kwa kuwa na wachezaji wenye uzoefu zaidi wanaojua namna ya kukabiliana na mazingira ya kutisha kama ya Uwanja wa St James’ Park ambako walicheza mechi wikiendi iliyopita dhidi ya Newcastle na kutoka sare ya mabao 2-2.
Newcastle ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 katika kipindi cha kwanza kabla ya Chelsea kusawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Reece James na Joao Pedro.
Licha ya kufahamu kuwa mkakati wa klabu hiyo umejikita kwa wachezaji vijana ambapo kwa sasa Chelsea ndio ina kikosi chenye wachezaji wenye umri mdogo zaidi kwenye Ligi Kuu England, Maresca amesema bado anaamini uwepo wa wachezaji wakongwe ungeisaidia timu kukabiliana na mechi ngumu.
"Bila shaka," amesema Maresca alipoulizwa kama angefanya vizuri angekuwa na wachezaji wakubwa zaidi katika kikosi.
"Unajua ni kwa sababu huenda wao wanajua zaidi namna ya kucheza kwenye uwanja wenye kelele au mazingira fulani. Wale tulio nao kwa sasa wanafanya kazi nzuri pia katika hilo. Hata hivyo, niseme tu hata hawa ambao wapo katika timu kwa sasa wanafanya vizuri. Ukiangalia katika mechi leo (wikiendi dhidi ya Newcastle), walionyesha ukomavu wa kutulia na kurudisha mabao yote mawili."
Maresca alionyeshwa kadi ya njano katika mechi hiyo na taarifa zinaeleza atalazimika kutumikia adhabu ya kusimamishwa mechi moja, ikiwa na maana atakaa jukwaani wakati Chelsea itakapokutana na Aston Villa kwenye Ligi Kuu huko Stamford Bridge Jumamosi ya wiki hii.
Matokeo hayo ya sare yalikuja katika kipindi kigumu ambacho mustakabali wa Maresca umekuwa ukijadiliwa na uongozi wa timu hiyo ambao unadaiwa kutompa sapoti ya kutosha kwa sasa huku baadhi yao wakihitaji aondoke.
"Wiki hii haikuwa ngumu kwangu. Ilikuwa nzuri. Tuliifunga Everton, tukaifunga Cardiff, na leo tumepata sare ugenini dhidi ya Newcastle. Nimefurahi na ninaamini tutafanya vizuri zaidi."