Maresca anajifanya haitaki Man City
Muktasari:
- Ripoti za hivi karibuni zilifichua kocha huyo Mtaliano yupo kwenye rada za Man City wakimtazama kama mtu mwafaka wa kwenda kuchukua mikoba ya Guardiola.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amesema haondolewi kwenye mfumo kutokana na kuhusishwa na kibarua cha kwenda kuinoa Manchester City kurithi mikoba ya Pep Guardiola wakati atakapoondoka.
Ripoti za hivi karibuni zilifichua kocha huyo Mtaliano yupo kwenye rada za Man City wakimtazama kama mtu mwafaka wa kwenda kuchukua mikoba ya Guardiola.
Hatima ya Guardiola huko Etihad bado haijawekwa wazi, ambapo mwakani itakuwa mwaka wake wa 10 katika klabu hiyo. Maresca aliwahi kufanya kazi chini ya Guardiola kama msaidizi wake na alikuwa kocha wa Man City pia katika timu ya vijana chini ya miaka 23 kabla ya kwenda kuinoa Leicester City.
Maresca alibainishwa anapewa nafasi kubwa ya kwenda kuvaa viatu vya Guardiola, lakini Mtaliano huyo alisema kwa sasa amekuwa na furaha kubwa kwenye klabu ya Chelsea na kulinganisha taarifa hizi na zile zilizomhusisha na Juventus.
Akizungumza kabla ya Chelsea kumenyana na Newcastle United Jumamosi, Maresca alisema: "Wala hainisumbui.
"Natambua huu ni uvumi kwa asilimia 100 kwa sasa, hakuna muda wa hii kitu. Nina mkataba Chelsea hadi 2029 na akili yangu ipo kwenye klabu hii. Najivunia kuwa hapa. Hizo nyingine ni uvumi tu. Wiki moja iliyopita, zilikuwa kama hivi zikihusisha Juventus, hivyo sizijali. Nasema tena, huu ni uvumi tu.
"Muhimu ni kuelewa kwanini kuna habari kama hizi, lakini sio kazi yangu. Sijali kitu, akili yangu ipo kwenye mchezo wa Newcastle." Maresca alipoulizwa kama atabaki Stamford Bridge hadi msimu ujao, alijibu hilo halina mjadala kwa sababu mkataba wake kwenye kikosi cha The Blues utafika tamati 2029.