Enzo Maresca aanza kutajwa Man City
Muktasari:
- Guardiola, ambaye ana mkataba na Man City hadi 2027, amewahi kudokeza suala la kuhitaji kupumzika baada ya kumaliza mkataba wake na klabu hiyo ya jijini Manchester.
Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, ametajwa kama kocha ambaye anaweza kuchukua nafasi ya Pep Guardiola endapo Mhispania huyo ataondoka katika kikosi cha Manchester City msimu ujao.
Guardiola, ambaye ana mkataba na Man City hadi 2027, amewahi kudokeza suala la kuhitaji kupumzika baada ya kumaliza mkataba wake na klabu hiyo ya jijini Manchester.
Vyanzo vya habari nchini Hispania, vinadai uwezekano wa Guardiola kuondoka Man city unaongezeka, ingawa uongozi wa klabu hiyo unahitaji kuendelea kufanya naye kazi.
Maresca ana historia na Man City, baada ya kujiunga na kikosi cha maendeleo mwaka 2020, kisha akawa kocha wa timu ya Serie B, Parma, kabla ya kurudi Etihad mwaka 2022 kama msaidizi wa Guardiola.
Alijiunga na Chelsea kuwa kocha mkuu mwaka 2024 baada ya kuipa mafanikio Leicester City iliyokuwa inashiriki Championship.
Maresca alimaliza nafasi ya nne msimu wa kwanza akiwa na Chelsea, huku akiiwezesha klabu hiyo ya jijini London kutwaa ubingwa wa Uefa Conference League na Fifa Club World Cup.
Kwa sasa Chelsea ipo nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kucheza mechi 16, huku mkataba wa kocha huyo raia wa Italia ukitarajiwa kufikia kikomo mwaka 2029.