Mapambano haya ya masumbwi pesa mbele unaambiwa

LONDON, ENGLAND. KUIBUKA kwa mapambano ya masumbwi ya kibabe na ongezeko la mabondia maarufu kumefanya mchezo wa masumbwi duniani kuwa sehemu ya kupiga pesa ndefu sana.
Kwa sasa, pambano la ngumi linapopigwa, vyanzo vya pesa vinakuwa vingi, kuanzia kwenye malipo ya kulipia kwenye televisheni ili kuona pambano husika na wale wanaolipa viingilio, ili kwenda kushuhudia ngumi zikipigwa ulingoni mubashara.
Kutokana na hilo, mabondia mashuhuti kama Anthony Joshua, Tyson Fury kwa kipindi hiki wakiamua kupigana, basi pambano lao litaingiza pesa nyingi kama ilivyokuwa kwa mapambano kadhaa yaliyopita huko nyuma likiwamo lile la Floyd Mayweather na Manny Pacquiao.
Kwenye mchezo huo wa masumbwi duniani, kumeshuhudiwa mapambano yaliyovutia pesa nyingi, ikiwamo ya viingilio, malipo ya televisheni pamoja na malipo ya mabondia wenyewe wanaoonyesha kazi ulingoni.
Kutokana na hilo, haya hapa mapambano sita ambayo yametajwa kuwa yameingiza pesa nyingi zaidi wakati Anthony Joshua akijiandaa kuzipiga na Francis Ngannou katika pambano litakalofanyika Ijumaa hii huko Saudi Arabia. Hilo nalo linatajwa kuwa ni pambano la pesa ndefu.
Mshindi kwenye pambano hilo anaweza kupata nafasi ya kuzipiga na ama Tyson Fury au Oleksandr Usyk.
FLOYD MAYWEATHER VS. MANNY PACQUIAO - MEI 2015
Lilipachikwa jina la ‘Pambano la Karne’ ambapo pesa nyingi sana ilihusishwa. Pambano hilo lililofanyika mwaka 2015 lilikuwa na faida kubwa kwa mabondia kwa sababu mashabiki walikuwa tayari kufanya kila wanachokiweza kushuhudia mabondia Floyd Mayweather na Manny Pacquiao wakizichapa.
Kilichotokea kwenye pambano hilo ni kwamba Mayweather alishinda kwa pointi, lakini kilichovutia wengi ni namna pambano hilo lilivyouza na kuingiza pesa nyingi, kupitia malipo ya televisheni na viingilio kwenye Ukumbi wa MGM Grand Garden Arena, ambapo tiketi ilikuwa inaanzia Dola 1,500.
Mkwanja ulivyokuwa;
Televisheni: Pauni 333 milioni
Viingilio: Pauni 58.7 milioni
Mgawo wa Mayweather: Pauni 223.5 milioni
Mgawo wa Pacquiao: Pauni 122 milioni
Jumla: Pauni 678 milioni
FLOYD MAYWEATHER VS. CONOR MCGREGOR - AGOSTI 2017
Pambano hilo lilipachikwa jina la ‘The Money Fight’ wakati linatangazwa na haikushangaza kuona Mayweather anahusika tena kutokana na kupenda kupigana kwenye mapambano ya pesa ndefu. Safari hii alikipiga na Conor McGregor kwenye Ukumbi wa T-Mobile Arena, Paradise huko Nevada. McGregor alihama kutoka kwenye mchezo wa masumbwi ya vizimba (UFC) na kwenda kwenye ulingo wa masumbwi ya kawaida ili kukipiga na Mayweather, ambaye aliandikisha ushindi wake wa 50 katika pambano hilo. Mkwanja aliovuna bondia Mayweather ulizidi kumuimarisha kwenye orodha ya wanamichezo matajiri duniani.
Mkwanja ulivyokuwa;
Televisheni: Pauni 325 milioni
Viingilio: Pauni 44 milioni
Mgawo wa Mayweather: Pauni 223.5 milioni
Mgawo wa McGregor: Pauni 70 milioni
Jumla: Pauni 662.5 milioni
FLOYD MAYWEATHER VS. CANELO ALVAREZ - SEPTEMBA 2013
Mayweather kwa mara nyingine, huwa hafanyi mapambano yasiyokuwa na pesa za kutosha. Hakuna ubishi, Mayweather ni moja ya mabondia mahiri zaidi duniani. Mwaka 2013 Canelo hakuwa supastaa kihivyo, alipata nafasi ya kuzipiga na bondia mwenye umaarufu mkubwa. Kwenye pambano hilo, Mayweather aliibuka na ushindi wa pointi kwa mara nyingine, huku mashabiki zaidi ya 16,000 walivutiwa kwenda kulitazama huko MGM Grand.
Kwa namna ilivyo, bondia Mayweather ni mtu anayependa kuibukia kwenye mapambano ambayo akishapigana, haondoki na mkwanja wa kichovu, anapiga pesa ya maana.
Mkwanja ulivyokuwa;
Televisheni: Pauni 120 milioni
Viingilio: Pauni 20 milioni
Mgawo wa Mayweather: Pauni 65 milioni
Mgawo wa Canelo: Pauni 9.7 milioni
Jumla: Pauni 214.7 milioni
FLOYD MAYWEATHER VS. OSCAR DE LA HOYA - MEI 2007
Bila shaka si kitu kinachokushangaza kuona jina la Mayweather kwa mara nyingine. Bondia huyo ni maarufu sana na amekuwa na mashabiki wengi na ndio maana mapambano yake yamekuwa yakiwa ya pesa nyingi kwa sababu yanavutia wengi. Lakini, kwa mwaka 2007, bondia Oscar De La Hoya ndiye aliyekuwa na jina kubwa kwa wakati huo na ndio maana hata kwenye mgawo wake ulikuwa mkubwa ukilinganisha na aliovuna Mayweather. De La Hoya alilipwa zaidi ya mara mbili ya Mayweather.
Hata hivyo, De La Hoya akifurahia zaidi kulipwa pesa nyingi, Mayweather ndiye aliyeibuka mshindi na hapo kuliweka juu zaidi jina lake kwenye ulingo wa masumbwi na kuwa kivutio kwa mashabiki wengi wa mchezo huo.
Mkwanja ulivyokuwa;
Televisheni: Pauni 110 milioni
Viingilio: Pauni 15 milioni
Mgawo wa De la Hoya: Pauni 42 milioni
Mgawo wa Mayweather: Pauni 20 milioni
Jumla: Pauni 187 milioni
EVANDER HOLYFIELD VS. MIKE TYSON II - 1997
Walau sasa pambano hili halikumhusisha Mayweather. Kipindi hicho masumbwi yalipokuwa na watu haswa kwenye mchezo huo, ambapo mwaka 1997, kulipigwa pambano moja matata kwenye Ukumbi wa MGM Grand Garden Arena.
Pambano hilo liliwahusisha Evander Holyfied na Mike Tyson ambapo walirudiana, mashabiki walipata nafasi ya kushuhudia wakali hao wakionyeshana ubabe tena.
Tyson alichapwa na Holyfied mwaka 1996 hivyo alitaka pambano hilo lirudiwe, lakini liliishia kwa utata mkubwa, ambapo Tyson aliingia kwenye aibu kubwa. Bingwa huyo wa zamani wa dunia kwenye uzito wa juu, Tyson alimng’ata sikio Holyfield, sio mara moja, alifanya hivyo mara mbili na hivyo kubwagwa kwenye matokeo.
Kwa mashabiki waliolipa kupitia televisheni, pambano hilo lilipata watu wengi kwelikweli.
MKWANJA ULIVYOKUWA;
Televisheni: Pauni 81.4 milioni
Viingilio: Pauni 11.6 milioni
Mgawo wa Holyfield: Pauni 28.4 milioni
Mgawo wa Tyson: Pauni 24.3 milioni
Jumla: Pauni 145.7 milioni
Lennox Lewis vs. Mike Tyson - 2002
Tyson alikaza misuli na kupigana na bondia Mwingereza, Lennox Lewis mwaka 2002, ambapo kwa kipindi hicho Lewis alikuwa bondia matata kabisa wa ubingwa wa uzito wa juu. Kwa ubora wake ndani ya ulingo, Lewis alishinda pambano hilo kwenye raundi ya nane.
Ushindi huo kwa Lewis ulikuwa mshtuko mkubwa kwa mashabiki, lakini kitu ambacho hakikuwa tofauti ni kwamba mabondia wote walipata mgawo sawa. Pambano lenyewe lilivutia mashabiki 15,000 waliofurika kwenye Ukumbi wa Pyramid Arena, Memphis huko Tennessee.
Kwenye orodha ya mabondia waliopigana kwenye mapambano yaliyovutia pesa nyingi, Tyson ametokea mara mbili, lakini Mayweather ameonekana kuwa mwamba zaidi, akichomoza kwenye mapambano manne tofauti.
MKWANJA ULIVYOKUWA;
Televisheni: Pauni 90 milioni
Viingilio: Pauni 14.2 milioni
Mgawo wa Lewis: Pauni 14.2 milioni
Mgawo wa Tyson: Pauni 14.2 milioni
Jumla: Pauni 132.6 milioni.