Mane, Pogba usajili wa majanga 2022-23

LONDON, ENGLAND. KILA kwenye usajili wa mastaa wakubwa, kuna ule ambao mambo yanakuwa hayaendi vizuri. Lakini, ushafahamu ni usajili gani mkubwa uliobeba matarajio makubwa lakini umekuwa na matokeo ya hovyo msimu huu huko Ulaya?
Kutokana na klabu kupata pesa nyingi, basi zenyewe zimekuwa zikifungulia pochi bila ya kujali kiwango cha pesa wanachotoa ili tu wanase mastaa inaowataka wakaongeze nguvu kwenye vikosi vyao.

Kwa msimu wa 2022-23 kuna dili za mastaa kibao zilizobeba matarajio makubwa kwenye ligi za Serie A, Bundesliga, La Liga, Ligue 1 na Ligi Kuu England - lakini mambo yamekuwa tofauti ndani ya uwanja na kuibua mijadala - wapewe muda au watupwe nje tu?


5. Antony (Man United, Pauni 85 milioni)
Kama kuna kitu Ajax inajua, basi ni kupiga bei mastaa wake. Moja ya mastaa wake iliyowauza ni Antony kwenda Manchester United mwaka jana kwa Pauni 85 milioni. Saini yake ilibeba matarajio makubwa. Baada ya kufunga bao kwenye mechi yake ya kwanza katika Ligi Kuu England, tena dhidi ya Arsenal, akaongeza matarajio. Lakini, baada ya hapo hakukuwa na maajabu mengine kutoka kwake kuendana na matarajio na pesa iliyotumika kumsajili.


4. Sadio Mane (Bayern Munich, Pauni 35milioni)
Sadio Mane alipaswa kuwa mtu wa kwenda kuziba pengo la Robert Lewandowski huko Allianz Arena, lakini msimu wake wa kwanza utakumbukwa zaidi kwa kumchapa ngumi mchezaji mwenzake, Leroy Sane. Mambo yake huko Bayern Munich hayakwenda vizuri kabisa na kuelezwa kwamba ndiyo sababu ya kufutwa kazi kwa kocha Julian Nagelsmann huku ikielezwa hakuwa vizuri pia na Thomas Tuchel. Mane hakuwa yule wa Liverpool huko Bayern.


3. Mykhailo Mudryk (Chelsea, Pauni 88.5milioni)
Chelsea ilipolipa Pauni 88.5 milioni kunasa saini ya Mykhailo Mudryk waliamini kuna mambo matamu yatatokea kwenye kikosi chao, lakini kilichowakuta kwenye Ligi Kuu England ni balaa zito, staa huyo ameshindwa kufanya jambo lolote la maana na timu ikamaliza nafasi ya 12 na kukosa tiketi ya michuano yote ya Ulaya. Mudryk anaonekana kama mchezaji aliyenunuliwa kwa pesa nyingi tofauti na uwezo wake wa uwanjani. Hakuwa na maajabu.


2. Richarlison (Tottenham, Pauni 60milioni)
Richarlison wakati anatua Tottenham Hotspur kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kulikuwa na imani kubwa kwamba timu hiyo ingeanza kushindania ubingwa chini ya kocha Antonio Conte. Lakini, mambo yamekuwa tofauti, Conte akapoteza imani na Mbrazili huyo. Richarlison alishindwa kujihakikishia nafasi Spurs hata katika msimu ambao Son Heung-min hakuwa bora uwanjani. Pesa iliyolipwa kumsajili ikaonekana ni hasara.


1. Paul Pogba (Juventus, bure)
Juventus wanaweza kujiona na mikosi kwa kumrudisha Paul Pogba kwenye kikosi chao kutoka Manchester United. Sawa, Pogba anaweza asilaumiwe kwa sababu mwili wake ndio uliomsaliti, lakini jambo hilo haliwezi kuondoa ukweli kwamba yeye ni miongoni mwa mastaa wakubwa waliotarajiwa kufanya vizuri msimu huu, lakini mambo yamekuwa tofauti. Na kinachoelezwa ni kwamba Pogba anaweza kuhama Juventus mwisho wa msimu huu.