Manchester United kuingilia dili la Rabiot

Muktasari:
- Licha ya wawakilishi wa staa huyu bado wapo katika mazungumzo na Liverpool, inaelezwa Man United inajaribu kuingilia kati dili hilo ikiamini itakuwa ni rahisi kumpata huyu ukilinganisha na Manuel Ugarte ambaye mambo yanaonekana kuwa magumu kutokana na pesa ambazo PSG inazihitaji ili kumuuza.
BAADA ya siku chache zilizopota taarifa mbalimbali kufichua kwamba kiungo wa zamani wa Juventus ambaye kwa sasa yupo huru Adrien Rabiot amefanya makubaliano na Liverpool na anatarajiwa kuwasili England kwa ajili ya vipimo vya afya, Man United imeingilia kati dili hilo na inamshawishi Rabiot abadili uamuzi na atue katika kikosi chao.
Licha ya wawakilishi wa staa huyu bado wapo katika mazungumzo na Liverpool, inaelezwa Man United inajaribu kuingilia kati dili hilo ikiamini itakuwa ni rahisi kumpata huyu ukilinganisha na Manuel Ugarte ambaye mambo yanaonekana kuwa magumu kutokana na pesa ambazo PSG inazihitaji ili kumuuza.
Man United inatarajiwa kuachana na Scott McTominay na Casemiro wote katika dirisha hili, hivyo inahitaji kusajili viungo wengine watakaokwenda kusuka upya eneo hilo.
Rabiot mwenyewe ameonyesha kutamani kutua Man United ingawa makubaliano na Liverpool tayari yameshafikiwa.
Katika kuhakikisha wanalohitaji linafanikiwa Man United imepanga kuweka ofa ya mshahara mnono zaidi ya ule ambao kiungo huyo amewekewa na Liverpool.
Wakati huo huo Lille inataka kumsajili beki wa West Ham na Morocco, Nayef Aguerd, 28, akawe mbadala wa Leny Yoro aliyejiunga na Manchester United latika dirisha hili.
Katika kufanikisha mchakato wa kumsajili staa huyu, Lille italazimika kutoa zaidi ya Pauni 30 milioni kama ada ya uhamisho. Mkataba wa Aguerd unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
CHELSEA inataka kumtoa tena kwa mkopo kiungo wao raia wa Brazil Andrey Santos, 20, kwenda Strasbourg katika dirisha hili baada ya kocha wao Enzo Maresca kuwaambia hayupo katika mipango yake kwa msimu ujao.
Staa huyu ambaye alijiunga na Chelsea katika dirisha la majira ya baridi mwaka jana, msimu uliopita alitolewa kwa mkopo kwenda Nottingham Forest na Strasbourg.
EVERTON inajiandaa kuwasilisha ofa kwenda Manchester City kwa ajili ya kumsajili kiungo wa timu hiyo na England, Kalvin Phillips, 28, katika dirisha hili.
Phillips ambaye mkaraba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, haonekani kuwa katika mipango ya kocha Pep Guardiola kwa msimu ujao.
ASTON Villa ipo tayari kumuuza beki wao raia wa Ufaransa, Lucas Digne, 31, katika dirisha hili kwa kile kinachoelezwa kwamba hatokuwa na nafasi ya kucheza baada ya timu hiyo kumsajili Ian Maatsen kutoka Chelsea kwa ajili ya kucheza nafasi yake.
Digne mwenye umri wa miaka 31, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026. Msimu uliopita alicheza mechi 46 za michuano yote.
ARSENAL imerudi mezani kwa Wolves na ofa nyingine mpya ili kuipata saini ya kipa wa timu hiyo Dan Bentley, katika dirisha hili.
Inaelezwa mabosi wa Wolves wanahitaji kiasi kisichopungua Pauni 1 milioni ili kumuuza kipa huyo wakati Arsenal ikidaiwa kuwasilisha ofa yapili ya Pauni 300,000 tu.
Kipa huyo wa zamani wa Brentford na Bristol City mkataba wake na Wolves unamalizika mwakani.
MANCHESTER City inataka kuwatoa Oscar Bobb na Rico Lewis kwa mkopo kwenda Newcastle United kwa ajili ya kurahisisha dili la kumsajili kiungo wa timu hiyo Bruno Guimaraes, katika dirisha hili.
Newcastle inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 100 milioni kwa ajili ya kumuuza Bruno na Man City inaona kiasi hicho ni kikubwa hivyo inawatoa mastaa hao ikiamini Newcastle itakubali kushusha bei kufikia Pauni 80 milioni.
LIVERPOOL inamfukuzia winga wa Real Sociedad, Takefusa Kubo, ili kumsajili kaitka dirisha hili na kwa mujibu wa ripoti dili hilo linaweza kumfanya Kubo kuwa mmoja kati ya wachezaji ghali zaidi kuwahi kutokea Japan.
Staa huyu wa kimataifa wa Japan, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.