Manchester City yajitosa dili la Marc Guehi
Muktasari:
- Mkataba wa sasa wa fundi huyu unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na Palace inataka kumuuza January kwa sababu amekataa kusaini mkataba mpya hivyo inahofia kuona akiondoka akiwa huru.
MANCHESTER City ni miongoni mwa tinu zinazohitaji saini ya beki kisiki wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England Marc Guehi mwenye umri wa miaka 25.
Guehi ni miongoni mwa wachezaji wanaowindwa na timu nyingi kubwa Ulaya dirisha lijalo la majira ya baridi.
Mkataba wa sasa wa fundi huyu unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na Palace inataka kumuuza January kwa sababu amekataa kusaini mkataba mpya hivyo inahofia kuona akiondoka akiwa huru.
Man City inamwona fundi huyu kama sehemu ya mipango yao ya muda mrefu ya kusuka kikosi chao ambacho kwa misimu miwili ya hivi karibuni kimeonekana kuwa katika hali mbaya.
Liverpool ndiyo inatajwa kuwa na nafasi nzuri ya kuipata saini yake na dirisha lililopita ilikuwa karibu kufanikisha hilo kabla ya dili kufeli katika dakika za mwisho baada ya kocha wa Palace kuzuia.
Mabosi wa Man City wanaweza kuwasilisha ofa nono January ili kuzipiku timu nyingine zinazoiwinda huduma ya staa huyu ambaye ameshaonyesha kuwa tayari kuondoka ikiwa Palace itakubali kumuuza.
Daniel Munoz
VIGOGO wa Ligi Kuu England, Manchester City, Manchester United na Chelsea wanaendelea kumfuatilia kwa karibu beki wa pembeni wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Colombia, Daniel Munoz mwenye umri wa miaka 29.
Inaelezwa timu hizi zinamfuatilia Munoz kwa sababu zinataka kuwasilisha ofa ya kumsajili dirisha lijalo la Januari.
Hata hivyo, Crystal Palace wamesisitiza hawana mpango wa kumwachia nyota huyo kwa sasa kutokana na umuhimu wake kikosini.
Conor Gallagher
MANCHESTER United bado ina mpango wa kumsajili kiungo wa Atletico Madrid, Conor Gallagher dirisha la usajili la Januari. Gallagher, 25, anatajwa kuwa kwenye orodha ya vipaumbele vya Man United dirisha lijalo.
Hata hivyo, baadhi ya ripoti zinaeleza Atletico haihitaji kumwachia fundi huyu. Staa huyu wa kimataifa wa England, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Tyler Adams
KIUNGO wa Bournemouth na timu ya taifa ya Marekani, Tyler Adams mwenye umri wa miaka 26, ametajwa kuwa katika rada za Manchester United inayohitaji kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kiwango cha Tyler alichoonyesha tangu msimu uliopita akiwa na Bournemouth. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 16 za michuano yote.
Kobbie Mainoo
NAPOLI pamoja na zaidi ya timu 10 za Ligi Kuu England zinaonyesha nia ya kumsajili kiungo wa Manchester United, Kobbie Mainoo mwenye umri wa miaka 20.
Hata hivyo, viongozi wa juu wa Manchester United wanasita kumwacha mchezaji huyo kwani bado wanaamini anaweza kuwa tegemeo katika kikosi chao kwa msimu ujao.
Licha ya kuzuiliwa kuondoka tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Mainoo amekuwa hapewi nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha mashetani hao wekundu chini ya kocha Ruben Amorim.
Lorenzo Torriani
ARSENAL inataka kumsajili kipa wa AC Milan na timu ya taifa ya Italia, Lorenzo Torriani, 20.
Maskauti wa washika mitutu hao wa Jiji la London wanadaiwa kumwangalia staa huyo kwa muda sasa na wameandika ripoti inayopendekeza asajiliwe baada ya kuridhishwa na kiwango bora alichoonyesha.
Awali kinda huyu alionekana kama mbadala sahihi wa Mike Maignan anayetarajiwa kuondoka mwisho wa msimu huu lakini sasa mambo yamebadilika na Milan itatakiwa kutafuta mbadala wake ikiwa itakubali kumuuza kwenda Arsenal.
Matt Targett
NEWCASTLE United inafikiria kumrejesha mapema beki wao wa kushoto raia wa England, Matt Targett, 30, ambaye anacheza kwa mkopo Middlesbrough inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza.
Mpango wa Newcastle kutaka kumrudisha Targett ambaye alisaini mkataba wa mkopo wa msimu mmoja kuitumikia Middlesbrough umechochewa na majeraha ya beki wao Dan Burn mwenye umri wa miaka 33 ambaye atakosekana kwa muda hali inayomlazimu kocha kutafuta chaguo mbadala haraka.
Ibrahim Konate
LIVERPOOL imeendelea kufanya mazungumzo na wawakilishi wa beki wao wa kimataifa wa Ufaransa, Ibrahim Konate ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Awali iliripotiwa Konate amekataa kusaini mkataba mpya na anataka kuondoka mwisho wa msimu.
Ilionekana huenda Liverpool ikakubali kumuuza Januari ili kupata pesa badala ya kukaa naye hadi mwisho wa msimu kisha kushuhudia akiondoka bure.
Hata hivyo, Liverpool inaonekana kutojali na imepanga kutomuuza Januari badala yake itafanya mazungumzo ili akubali ofa yao.