MAN UNITED YATUPWA NJE CARABAO

Thursday September 23 2021
maan pic

LONDON, ENGLAND. MASHETANI wekundu wa Old Trafford, Manchester United   wametupwa nje ya Kombe la Ligi ya  England ambalo ni maarufu kama Carabao baada ya kukubali kipigo usiku wa jana, Jumatano  cha bao 1-0 dhidi ya wagonga nyundo wa London, West Ham United.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Manuel Lanzini ndiye aliyeifanya West Ham kuibuka na ushindi wake wa kwanza kwenye uwanja wa  Old Trafford tangu  2007 na kuwafanya Manchester United kufangasha virago vyao kwenye michuano hiyo ambayo misimu miwili iliyopita walitinga hatua ya nusu fainali.

Katika mchezo huo, kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer  alitoa nafasi kwenye kikosi chake cha kwanza kwa  Jadon Sancho na Anthony Martial  kuongoza mashambulizi ya timu hiyo lakini walionekana kuchemka ikabidi kuwaingiza  Mason Greenwood na Bruno Fernandes.

Licha ya mabadiliko hayo, West Ham ambayo iliwapumzisha baadhi ya nyota wao muhimu kama vile  Tomas Soucek, Declan Rice na Michail Antonio walionekana kuwa imara na kumudu presha ya mashambulizi ya Manchester United ambao walikuwa wakisaka bao la kusawazisha.

Wakati Manchester United ikitupwa nje ya michuano hiyo wenzao, Manchester City wametinga raundi ya nne baada ya kuishushia kipigo     Wycombe Wanderers cha mabao 6-1, Arsenal nao waliitandika  AFC Wimbledon mabao 3-0, Chelsea wamevuka raundi ya tatu baada ya kuifunga Aston Villa kwa penalti 4-3 baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Upande mwingine Liverpool wakiwa ugenini waliitandika Norwich mabao 3-0, kama ilivyokuwa kwa Chelsea, Tottenham nao wametinga raundi ya nne kwa penalti 3-2 baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya wenyeji wao, Wolverhampton Wanderers.

Advertisement

RATIBA YA RAUNDI YA NNE
Chelsea  v    Southampton  
Arsenal  v    Leeds United
QPR   v  Sunderland  
Stoke City v  Brentford
West Ham  v Manchester City
Leicester City  v  Brighton   
Burnley      v  Tottenham Hotspur  
Preston North End     v  Liverpool  
 

Advertisement