Man United yafuta sherehe za tuzo

Muktasari:
- Utamaduni wa Man United ni kuandaa sherehe kubwa uwanjani Old Trafford kila mwisho wa msimu kwa ajili ya kutoa tuzo kwa wachezaji wa timu za kiume na kike kwa wale waliofanya vizuri, ikiwamo tuzo ya Sir Matt Busby inayotolewa kwa mchezaji bora wa mwaka.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imefuta sherehe za mwisho wa msimu za kupeana tuzo pamoja na kupata mlo wa pamoja baada ya timu hiyo kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu England.
Utamaduni wa Man United ni kuandaa sherehe kubwa uwanjani Old Trafford kila mwisho wa msimu kwa ajili ya kutoa tuzo kwa wachezaji wa timu za kiume na kike kwa wale waliofanya vizuri, ikiwamo tuzo ya Sir Matt Busby inayotolewa kwa mchezaji bora wa mwaka.
Lakini, kikosi hicho kinachonolewa na Mreno Ruben Amorim kinashika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, kimeamua kufuta usiku huo wa tuzo kwa sababu wanaona hauna maana kwa kipindi hiki licha ya Man United kutinga fainali ya Europa League.
Timu ya soka ya wanawake ya Man United imemaliza nafasi ya tatu kwenye ligi ya WSL, ikifuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati timu ya vijana ya Man United imemaliza nafasi ya tano kwenye Premier League 2 na ile ya chini ya miaka 18 imemaliza nafasi ya pili kwenye ligi yao.
Badala ya mlo wa usiku, sasa tuzo za wachezaji waliofanya vizuri kwenye kikosi cha wakubwa watakabidhiwa uwanjani Old Trafford kabla ya mechi yao ya mwisho wa msimu kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Aston Villa.
Kiungo na nahodha wa timu hiyo, Bruno Fernandes ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka na kama atabeba basi itakuwa kwa mara ya nne. Hii ni mara ya tatu katika misimu minne ya mwisho sherehe hizo kufutwa, ambapo Man United iliona pia hakuna maana ya kufanya sherehe ilipomaliza katika nafasi ya nane katika Ligi Kuu chini ya Erik Ten Hag.
Ilifuta sherehe za aina hiyo kwenye msimu wa 2021-22 ilipomaliza nafasi ya sita kwenye ligi ikikusanya pointi 58 na hivyo kumshuhudia kocha Ole Gunnar Solskjaer akifutwa kazi.
Man United msimu huu imekusanya pointi 39 katika mechi 36 na kukumbana na vichapo 17.