Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mamelodi Sundowns yatetea ubingwa PSL

Muktasari:

  • Kocha wa Mamelodi, Miguel Cardoso ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutokea Ureno kutwaa taji la Ligi Kuu Afrika Kusini.

PRETORIA, AFRIKA KUSINI: Mamelodi Sundowns (Masandawana) wameendeleza ubabe kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) baada ya kutwaa tena ubingwa msimu huu wa 2024-2025 kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Chippa United katika mchezo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Buffalo City.

Huu ni ubingwa wa nane mfululizo kwa Masandawana, na wa 17 kwa jumla, hatua inayowafanya kuwa klabu yenye mataji mengi zaidi ya Ligi katika historia ya Afrika Kusini, wakiizidi miamba kama Kaizer Chiefs (mataji 13) na Orlando Pirates (mataji 9).

Katika mchezo huo, Iqraam Rayners aliwapa uongozi Mamelodi ambao walikuwa wageni akifunga bao katika dakika ya 10, likiwa ni bao lake la 14 msimu huu, Arthur Sales aliingia kipindi cha pili akifunga mabao mawili, moja katika dakika ya 69 na jingine dakika ya 89 baada ya kipa wa Chippa United, Darren Johnson kufanya kosa la kizembe.

Ubingwa huu unaifanya Sundowns kuendeleza ubabe wa kutwaa mataji manane mfululizo katika Soka la Afrika Kusini tangu walipoanza kuchukua taji hilo msimu wa 2017-2018, ikiwa chini ya makocha wanne tofauti. Pitso Mosimane (mataji matatu), Rhulani Mokwena (mataji manne) na sasa Miguel Cardoso (taji moja).

Kocha wa Mamelodi, Miguel Cardoso ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutokea Ureno kutwaa taji la Ligi Kuu Afrika Kusini.

"Tunapaswa kusherehekea kwa mbwembwe kwa sababu kuna rekodi tumezivunja, nafikiri historia imeandikwa. Tamaa ni jambo muhimu katika mchezo wa soka, tunaendelea kujipanga na mchezo wa fainali katika Ligi ya Mabingwa," amesema Miguel Cardoso Kocha wa Sundowns.

Hlompho Kekana, aliyestaafu mwaka 2021, bado anaongoza kwa kutwaa mataji mengi ya Ligi akiwa na Sundowns ambapo alitwaa mataji sita akicheza katika nafasi ya kiungo na kuwa nahodha kwa muda mrefu.

Wachezaji kadhaa wa kikosi cha sasa wameonja utamu wa taji la ligi hiyo kwa mara ya kwanza ambao ni Lucas Suarez, Matias Esquivel, Iqraam Rayners pamoja na kinda, Abram Mashele, aliyepewa nafasi kwenye kikosi cha wakubwa akitokea akademi.

Baada ya kutwaa taji la ligi hiyo sasa Mamelodi Sundowns wana nafasi ya kutwaa taji lingine kwani watacheza mchezo wa fainali ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Pyramids, Mei 24 mwaka huu ambapo wataanzia kwenye dimba la nyumbani na kumalizia ugenini Juni, Mosi mwaka huu.