CAF yadaiwa kuiondoa Simba, Berkane Kwa Mkapa

Muktasari:
- Taarifa ambayo Simba imeshaipokea ni kwamba CAF imeliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanza kuhamisha maandalizi yote ya fainali hiyo ya pili kwenye Uwanja wa Mkapa na sasa yahamie New Amaan, Zanzibar.
TAARIFA mbaya kwa Simba ni kwamba, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), imedaiwa kuwa, limeuondoa mchezo wa fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na RS Bekrane kupigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Taarifa ambayo Simba imeshaipokea ni kwamba CAF imeliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanza kuhamisha maandalizi yote ya fainali hiyo ya pili kwenye Uwanja wa Mkapa na sasa yahamie New Amaan, Zanzibar.
Taarifa hiyo, imekuwa ni kama pigo kubwa kwa Simba ambayo ina rekodi kubwa ya ushindi kwenye Uwanja wa Mkapa kwani ya mwisho kupoteza uwanjani hapo ni Machi 29 mwaka jana ilipolala 1-0 mbele ya Al Alhy ya Misri katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, Simba na TFF bado zinaendelea kupambana kubadilisha maamuzi hayo ya CAF kwa maombi maalum juu ya mechi hiyo ya kihistoria.
Si Simba pekee iliyotibuliwa na CAF, mapema wiki iliyopita Shirikisho hilo, lilizuia Uwanja wa Nyayo, uliopo Kenya kutumika kwa pambano la Dabi ya Mashemeji kati ya AFC Leopards na Gor Mahia ikihofia uwanja huo kuharibika kwa matumizi ya Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Fainali hizo za CHAN kwa mwaka huu, zitachezwa katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania kuanzia Agosti mwaka huu.
CAF imekuwa kwenye usimamizi mkubwa wa viwanja hivyo, kutokana na bado vinaendelea na maboresho kwa matumizi ya Fainali hizo za CHAN na baadaye AFCON.