Man United waambiwa Casemiro asiondoke
Muktasari:
- Hivi karibuni ilitangazwa Casemiro ataondoka Old Trafford baada ya kucheza misimu minne. Kiungo huyo alinunuliwa kwa Pauni 70 milioni wakati miamba hiyo ilipokuwa chini ya Kocha Erik ten Hag.
MANCHESTER, ENGLAND: NGULI wa Manchester United, Bryan Robson ameitaka klabu hiyo kubadilisha uamuzi wao kuhusu Casemiro na kumbakiza baada ya msimu huu, akisisitiza bado ni mchezaji bora ambaye anaweza kuongeza mchango zaidi kwa timu.
Hivi karibuni ilitangazwa Casemiro ataondoka Old Trafford baada ya kucheza misimu minne. Kiungo huyo alinunuliwa kwa Pauni 70 milioni wakati miamba hiyo ilipokuwa chini ya Kocha Erik ten Hag.
Katika kipindi chake Man United, Casemiro alipitia nyakati tofauti alianza kwa kiwango cha juu sana kabla ya kiwango chake kushuka. Hata hivyo, msimu huu ameonyesha kurejea katika kiwango kizuri baada ya kuthibitisha mpango wake wa kuondoka kwenye timu hiyo.
Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid ameshinda taji mara kibao la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Licha ya kuwa na umri wa miaka 34, bado ana uwezo mkubwa wa kusaidia timu.
Robson anaamini Man United inapaswa kufikiria upya uamuzi wao kwa sababu Casemiro bado ana mengi ya kutoa, ingawa hali ya kutokuwa wazi kuhusu nafasi ya kocha wa kudumu inaweza kuathiri maamuzi hayo.
Robson alisema: “Ningemshauri Casemiro abaki. Amekuwa na msimu mzuri sana mwaka huu. Ni mchezaji bora. Ana akili kubwa ya soka. Ana uwezo mzuri wa kupiga pasi. Ana nguvu kwenye mipira ya juu na anapokaba anaonyesha nia ya kweli.
“Huwezi kukaa Real Madrid kwa miaka mingi na kushinda mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kama si mchezaji wa kiwango cha juu kabisa. Watu wanaona uwezo wake halisi. Nafikiri msimu ujao anaweza kutusaidia zaidi kwa uzoefu wake. Pia alikuwa mzuri sana barani Ulaya mwaka jana.”
Man United inapanga kuongeza angalau kiungo mmoja katika kikosi chao majira ya joto. Nafasi hiyo inaonekana kuwa moja ya maeneo ya kipaumbele. Hata hivyo, Casemiro amekuwa mchezaji muhimu tangu Michael Carrick alipoteuliwa kuwa kocha hadi mwisho wa msimu. Uzoefu wake umeonekana kuwa msaada mkubwa kwa timu na Carrick alisema: “Lazima niseme, Casemiro amekuwa mzuri sana tangu nilipoanza kazi, ndani na nje ya uwanja. Uzoefu ni kitu muhimu sana kama utakitumia kwa njia sahihi.”