Man United uhakika kwa Gyokeres

Muktasari:
- Gyokeres, mwenye umri wa miaka 27, alifunga mabao 54 katika mechi 52 msimu uliopita akiwa Sporting. Ingawa ana kifungu cha kuachiliwa kwa Pauni 85 milioni, inaelezwa timu yake iko tayari kumuuza kwa Pauni 60 milioni kutokana na ahadi waliyompa kama heshima baada ya staa huyu kukataa kuondoka Januari mwaka huu licha ya kuwekewa ofa nono.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United wamepiga hatua kubwa katika mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres na kuna uwezekano wakaipiku Arsenal katika mbio za kumnasa raia huyo wa Sweden.
Gyokeres, mwenye umri wa miaka 27, alifunga mabao 54 katika mechi 52 msimu uliopita akiwa Sporting. Ingawa ana kifungu cha kuachiliwa kwa Pauni 85 milioni, inaelezwa timu yake iko tayari kumuuza kwa Pauni 60 milioni kutokana na ahadi waliyompa kama heshima baada ya staa huyu kukataa kuondoka Januari mwaka huu licha ya kuwekewa ofa nono.
Man United wamepata matumaini ya kukamilisha dili la staa huyu baada ya kupata nafuu ya kifedha kutokana na hatua kali za kupunguza matumizi zilizoongozwa na mmiliki mwenza mpya, Sir Jim Ratcliffe na matumizi ya uendeshaji yameshuka kwa Pauni 41.6 milioni hadi Pauni 162.1 milioni kwa robo ya mwisho ya mwaka wa kifedha.
Arsenal nao wanamfuatilia kwa karibu Gyokeres, pia wameweka jicho kwa mshambuliaji wa RB Leipzig, Benjamin Sesko.
Kocha wa United, Ruben Amorim, aliyetokea Sporting, anaonekana kuwa na hamu ya kumrudisha mshambuliaji wake wa zamani kujiunga na kikosi chake kipya ndani ya Old Trafford.
Pamoja na matumaini hayo mapya, mzigo wa madeni uliosababishwa na Glazers bado ni mkubwa hali inayosababisha Ratcliffe kuendelea kubana matumizi kwa kuondoa zaidi wafanyakazi.
Mkurugenzi Mtendaji mpya, Omar Berrada, amekiri msimu uliopita ulikuwa wa aibu baada ya United kumaliza ligi wakiwa nafasi ya 15 na kupoteza fainali ya Europa League dhidi ya Tottenham, hivyo wanajipanga kufanya usajili utakaosaidia timu. “Tulijivunia kufika fainali ya Europa League lakini tulikatishwa tamaa baada ya kufungwa. Msimu wetu wa Ligi Kuu ulikuwa dhaifu sana na haukukidhi matarajio yetu. Tunatarajia maboresho makubwa msimu ujao.”
Man United tayari wamekubaliana na Wolves kuhusu usajili wa Matheus Cunha kwa Pauni 62.5 milioni na bado wanamwania Bryan Mbeumo wa Brentford.
Hata hivyo, Amorim atalazimika kuwaachilia baadhi ya wachezaji maarufu kama Marcus Rashford, Jadon Sancho, Alejandro Garnacho, Antony na Casemiro ili kufanikisha usajili mpya na kuweka uwiano mzuri wa kifedha.