Man United ina mambo 11 Europa League

Muktasari:
- Huo ulikuwa ushindi muhimu kwa kikosi hicho kinachonolewa na Ruben Amorim, ambapo sasa kitasubiri mechi ya marudiano itakayofanyika Old Trafford, Alhamisi ijayo kikitambua wazi ushindi kwenye kombe hilo ndio utakaokipa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya hali kuwa ngumu kwenye ligi ya ndani.
BILBAO, HISPANIA: MANCHESTER United imetanguliza mguu mmoja kwenye fainali ya Europa League baada ya kuibuka na ushindi mnono ugenini wa mabao 3-0 ilipokipiga na Athletic Bilbao katika nusu fainali ya kwanza.
Huo ulikuwa ushindi muhimu kwa kikosi hicho kinachonolewa na Ruben Amorim, ambapo sasa kitasubiri mechi ya marudiano itakayofanyika Old Trafford, Alhamisi ijayo kikitambua wazi ushindi kwenye kombe hilo ndio utakaokipa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya hali kuwa ngumu kwenye ligi ya ndani.
Kutokana na Tottenham Hotspur na yenyewe kushinda mechi ya kwanza ya nusu fainali, kuna uwezekano mkubwa wa kushuhudia fainali ya Europa League itakayokutanisha miamba miwili ya Ligi Kuu England uwanjani San Mames, Bilbao, Mei 17.

Athletic iliingia kwenye mechi ikipewa nafasi kubwa ya kuichapa Man United hasa kutokana na kiwango chake cha sasa, rekodi yake ya uwanja wa nyumbani na inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa La Liga. Lakini, baada ya dakika 90 za mchezo wa kwanza wa nusu fainali, ndoto za kucheza fainali ya Europa League itakayopigwa kwenye uwanja wake imekuwa ngumu kwa sasa, baada ya kukubali kipigo hicho kizito cha mabao 3-0 nyumbani. Bilbao ilianza kwa kuipa presha Man United, lakini bao la mapema la Alejandro Garnacho ambalo lilikataliwa na VAR kwa kuwa mfungaji alikuwa ameotea, ilikuwa ishara ya onyo la kwanza kwa wenyeji hao.
Kisha Harry Maguire alifanya mambo yake kwenye wingi ya kulia, wakati alipopiga krosi iliyokwenda kuzaa bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na Casemiro. Kuanzia hapo, Bilbao ikalegea. Man United iliongeza bao la pili kwenye mkwaju wa penalti ya Bruno Fernandes iliyotokana na uamuzi wa VAR kufuatia Dani Vivian kumshika Rasmus Hojlund ndani ya boksi na kwa kuwa alikuwa mtu wa mwisho, alionyeshwa kadi nyekundu na kutoka nje kuifanya Bilbao kucheza sehemu kubwa ya mechi ikiwa pungufu.
Muda mfupi kabla ya mapumziko, Fernandes aliifungia bao la tatu Man Uniteda baada ya pasi ya kisigino ya kiungo Manuel Ugarte. Kipindi cha pili, Man United ililinda vyema uongozi wake wa mabao hayo matatu na sasa inasubiri mechi ya marudiano itakayofanyika uwanjani Old Trafford ili kufahamu hatima ya kutinga fainali ya michuano hiyo.

Kutokana na kilichotokea kwenye mchezo huo wa San Mames, hizi hapa dondoo tamu za ushindi wa Man United.
1. Man United ilipiga mashuti 14 dhidi ya tisa ya wenyeji wao, huku mashuti saba yakilenga golini dhidi ya matatu ya Bilbao. Katika mechi hiyo, Man United ilimiliki mpira kwa asilimia 72.4 na kupiga pasi sahihi 558, huku Athletic ikipiga 160.
2. Man United inaendelea kuwa timu pekee ambayo haijapoteza kwenye michuano yote mitatu ya UEFA msimu huu. Imeshinda mechi nane na kutoka sare tano kati ya 13 ilizocheza kwenye Europa League.

3. Wakati mechi nyingine zikiwa za mtoano, wastani wa Man United wa pointi kwa mechi kwenye Europa League ni 2.23. Hiyo ni karibu mara mbili ya wastani wa pointi zao kwenye Ligi Kuu England kwa msimu huu, 1.14.
4. Man United imefunga mabao mengi kwenye Europa League mwaka 2025 (19) kuliko iliyofunga kwenye Ligi Kuu England (18) - licha ya kucheza mechi karibu mara mbili (15 kwa saba).
5. Opta iliipa Athletic Bilbao asilimia 48.8 ya kushinda mechi hiyo ya San Mames, wakati Man United ilipewa asilimia 25.5% kwenye utabiri wao uliofanywa kwa kompyuta kabla ya mechi hiyo kufanyika.
6. Beki Victor Lindelof alipiga pasi sahihi 95 wa upande wa Man United. Hiyo ilikuwa zaidi ya pasi 73 dhidi ya kinara wa pasi wa Athletic Bilbao, Yaray Alvarez, aliyepiga pasi 22.

7. Bilbao chini ya kocha Ernesto Valverde ilikuwa imepoteza mechi moja tu kati ya 17 za La Liga ilizocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani msimu huu. Na ni Atletico Madrid na Osasuna pekee zilizoshinda mara nyingi nyumbani kwa Bilbao (kwenye michuano yote) tangu kipigo chao cha 2-0 kutoka kwa Real Madrid mwanzoni mwa msimu uliopita.
8. Katika mechi 23 ilizocheza nyumbani kwenye La Liga na Europa League msimu huu, Athletic Bilbao imeruhusu mabao 12. Man United imewachapa mabao matatu ndani ya dakika 45.
9. Hakuna mchezaji kwenye historia ya Europa League ambaye amehusika kwenye mabao mengi (amefunga 19, asisti 12) kwenye mechi za mtoano kumzidi Bruno Fernandes. Nahodha huyo wa Man United amehusika kwenye mabao 31 katika mechi 32 za mtoano.

10. Mohamed Salah ni mchezaji pekee kwenye Ligi Kuu England ambaye amehusika kwenye mabao mengi kumzidi Fernandes (mabao 35, amefunga 19, asisti 16) katika michuano yote msimu huu 2024-25.
11. Kwa ushindi wa Spurs wa 3-1 dhidi ya Bodo/Glimt, dalili zinaonyesha kunaweza kutokea fainali ya timu mbili za Ligi Kuu England kwenye Europa League. Hiyo ilitokea mara moja tu kwenye historia ya Man United (fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2008 dhidi ya Chelsea) ambapo ilikutana na timu nyingine ya England katika fainali ya Ulaya.