Man United hapatoshi… Watatu watajwa
Muktasari:
- Amorim alipata kichapo chake cha 17 cha Ligi Kuu England wikiendi iliyopita baada ya kupoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Brentford.
MANCHESTER, ENGLAND: TAARIFA kutoka Manchester United zinadai Oliver Glasner, Fabian Hurzeler na Andoni Iraola ni miongoni mwa makocha wanaofikiriwa na mabosi wa timu hiyo kupewa mikoba ya Ruben Amorim ambaye huenda akafukuzwa.
Amorim alipata kichapo chake cha 17 cha Ligi Kuu England wikiendi iliyopita baada ya kupoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Brentford.
Hiyo ilikuwa ni mechi yake ya 33 ya EPL kusimama kama kocha wa Man United tangu ajiunge nayo mwaka jana.
Ingawa Amorim bado anaungwa mkono na uongozi wa klabu ambao wamemwambia wana imani naye, Man United inaendelea kufuatilia uwezekano wa kumpata mbadala wake ikiwa mambo yataendelea kuwa mabaya.
Vyanzo kutoka klabu hiyo vinasisitiza hawana mrithi rasmi aliyechaguliwa kama mbdala wa Amorim, lakini wanasisitiza wataanza mazungumzo na makocha wa kuchukua nafasi yake ikiwa timu itaendelea kufanya vibaya.
Msimu uliopita, Erik ten Hag alifutwa kazi baada ya kufungwa mechi nne kati ya tisa za mwanzo wa ligi, lakini safari hii uongozi wa Man United unaonekana kuwa wavumilivu zaidi.
Dirisha la usajili la majira ya kiangazi, Man United ilifanya usajili wa maboresho kwa kuchukua mastaa ambao tayari wana uzoefu wa ligi kama Matheus Cunha na Bryan Mbeumo.
Ikiwa itamfukuza Amorim, inafikiria pia kusajili kocha mwenye uzoefu wa ligi ili isichukue muda mrefu kuipa matokeo.
Mpango huo wa kuchukua kocha mwenye uzoefu wa ligi unadaiwa kumtupa nje ya mchakato kocha wa zamani wa timu ya taifa ya England Gareth Southgate ambaye hajawahi kufundisha klabu ya EPL tangu mwaka 2009 ambapo aliinoa Middlesbrough iliyoshuka daraja.
Glasner ambaye aliiwezesha Crystal Palace kushinda kombe lao la kwanza la FA msimu uliopita anapewa nafasi kubwa ya kuchukua mikona ya Amorim na amepata sifa zaidi baadaya kiwango bora ambacho Palace imekionyesha tangu kuanza kwa msimu huu ambapo haijapoteza mechi yoyote.
Iraola anayeifundisha Bournemouth aliyojiunga nayo miaka miwili iliyopita naye anapewa nafasi kwa uwezo wake wa kujenga timu kwani licha ya kupoteza wachezaji wake muhimu katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi ambao ni Dean Huijsen, Ilya Zabarnyi na Milos Kerkez, timu yake bado imeendelea kuwa imara na sasa inapambana katika nafasi tano za juu kwenye msimamo wa EPL.
Kocha Hurzeler anayeifundisha Brighton naye anatazamwa kama sehemu ya mkakati huo.