Man united, Arsenal zamtia wazimu Gyokeres

Muktasari:
- Straika huyo wa Sporting CP amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa ikiwamo Manchester United na Arsenal.
LISBON, URENO: VIKTOR Gyokeres ametishia kuingia kwenye mgomo ili kulazimisha kuuzwa dirisha hili la majira ya kiangazi, imeelezwa.
Straika huyo wa Sporting CP amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa ikiwamo Manchester United na Arsenal.
Gyokeres alisema kulikuwa na makubaliano na mabosi wa Sporting, Septemba mwaka jana, anaweza kuachana na timu hiyo kwa ada ya Pauni 60 milioni pamoja na nyongeza ndogo.
Kwa mujibu wa gazeti la Record la Ureno, staa huyo wa kimataifa wa Sweden alikasirishwa baada ya Sporting kupandisha bei ikihitaji kiwango kinachoanzia Pauni 70 milioni kwenda juu.
Ripoti hiyo ilibainisha Gyokeres alisisitiza hatachezea klabu hiyo tena kitu ambacho kimeonyesha dhamira yake ya kutaka kuhama dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Fowadi huyo wa zamani wa Coventry City aliripotiwa kuwaambia mabosi wa Sporting yupo tayari kuingia kwenye mgomo ili kulazimisha uhamisho. Gyokeres ana mkataba wa miaka mitatu katika klabu hiyo.
Kipengele kilichowekwa kwenye mkataba anaweza kuuzwa kwa Pauni 85 milioni na wakala wake inaaminika aliwaambia mabosi wa Sporting yupo kwenye rada za klabu nne ikiwamo Man United na Arsenal. Uhamisho wa kwenda Old Trafford utakamfanya kukutana na kocha wake wa zamani wa Sporting, Ruben Amorim. Arsenal nayo ipo kwenye vita ya kusaka straika baada ya Kocha Mikel Arteta kubainisha anasaka Namba 9. Timu nyingine ni Al-Hilal ya Saudi Arabia na Juventus ya Italia.
Gyokeres, 27, alikuwa kwenye kiwango bora msimu uliopita. Kinda huyo wa zamani wa Brighton alifunga mabao 39 katika mechi 33 kwenye ligi ya Ureno.
Gyokeres, ambaye alisema anahisi kusalitiwa na mabosi wa Sporting alisema kuhusu hatima yake: “Ni soka, bado nipo hapa. Sijui nini kitakwenda kutokea. Hakuna anayeweza kutabiri mambo ya baadaye.”