Man City v Liverpool ni bato la Haaland, Van Dijk
Muktasari:
- Ndiyo hivyo. Na bila shaka, usiku wa kuamkia Jumapili, ulikuwa wenye presha kubwa kwa beki wa kati wa Liverpoool, Virgil van Dijk.
MANCHESTER, ENGLAND: WASWAHILI wana msemo wao unasema hivi, usiku wa deni haukawii kucha.
Ndiyo hivyo. Na bila shaka, usiku wa kuamkia Jumapili, ulikuwa wenye presha kubwa kwa beki wa kati wa Liverpoool, Virgil van Dijk.
Unajua kwa nini? Anajua janga analokwenda kukabiliana nalo, linaitwa Erling Haaland.
Na mchambuzi mmoja wa soka, Steven McInerney amesema Haaland atakwenda kuwa tatizo kubwa kwa Van Dijk uwanjani Etihad, Jumapili endapo kama kocha Pep Guardiola atarudia mbinu zake alizozitumia katika mchezo dhidi ya Bournemouth.
Manchester City itajimwaga uwanjani Etihad kukabiliana na Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu England, unaotazamiwa kuwa na upinzani mkali katika mbio za kusaka ubingwa.
Namba 9 huyo wa Man City amekuwa kwenye kiwango bora sana katika Ligi Kuu England msimu huu, akifunga mabao 13 katika mechi 10. Kabla ya mechi za Jumamosi kwenye ligi hiyo, msimamo ulikuwa unasomeka, Man City ipo nafasi ya pili, pointi moja zaidi ya Liverpool kwenye namba tatu. Mechi hiyo itakuwa ya vuta nikuvute.
Kwenye michuano yote, Haaland amefunga mabao 18 katika mechi 14 alizochezea Man City, huku mabao 10 kati ya hayo, amefunga katka mechi saba zilizochezwa Etihad, ikiwamo mawili kwenye ushindi wa 3-1 kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Bournemouth wikiendi iliyopita.
Alifunga pia dhidi ya klabu yake ya zamani ya Borussia Dortmund, wakati Man City iliposhinda 4-1 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumatano iliyopita.
Haaland alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi baada ya kuonyesha kiwango bora dhidi ya Bournemouth na alikuwa kwenye mikimbio matata akisaidiwa na Phil Foden na Rayan Cherki kwenye safu ya ushambuliaji watatu wa Man City.
Kwa kiwango cha Man City na mbinu ilizotumia dhidi ya Bournemouth, ambao walikuwa kwenye kiwango bora wakiwa hawajapoteza mchezo wowote katika mechi nane kabla ya kwenda Etihad, McInerney anaamini Guardiola atakwenda kukabiliana na Liverpool kwa mtindo wa “copy and paste” ya mbinu zake alizotumia kwenye mechi ya Bournemouth.
Kama itakuwa hivyo, basi beki wa kati wa Liverpool, Van Dijk atakuwa kwenye wakati mgumu wa kukabiliana na mikimbio ya Haaland. Na kitu kibaya kwa Van Dijk kwa sasa, hayupo kwenye kiwango chake bora kabisa. Safu ya ulinzi ya Liverpool imekuwa kwenye wakati mgumu, huku ni mechi mbili tu ndizo ambazo ilicheza bila ya kuruhusu wavu wao kuguswa, dhidi ya Aston Villa (2-0) na Real Madrid (1-0).
Zaidi ya hapo, Liverpool imeruhusu mabao 22 katika mechi 14 ilizocheza kwenye michuano yote tangtu mwanzoni mwa msimu huu, huku mabao 14 ikikumbana nayo kwenye mechi tisa ilizocheza kwenye Ligi Kuu England, huku kukiwa na timu tatu tu ndizo zilizofungwa mabao mengi, 15 au zaidi.
Alipoulizwa kuhusu wachezaji wa Man City watakaotajwa kwenye mechi hiyo na kuanzishwa na Guardiola, McInerney aliambia Sports Mole: “Ningetumia Ctrl C, Ctrl V. Ningefanya copy and paste kikosi kilichocheza na Bournemouth dhidi ya Liverpool.
“Bournemouth ni timu nzuri kuliko Liverpool kwa sasa katika suala la kucheza kwa kiwango cha juu kwa muda mrefu na kuwa na staili yao ya kibabe. Nadhani kucheza nyumbani inaipa nguvu pia Man City.
“Kwenye suala la ubunifu, nadhani Foden, Haaland na Cherki watakuwa tatizo kubwa sana kwa Liverpool. Nadhani itakuwa balaa kubwa na Bernardo Silva anaichukia kwelikweli Liverpool.”
Kwenye namba, hii itakuwa mechi ya 56 kwa miamba hiyo kukutana kwenye ligi, mara 21 zilimalizika kwa sare, huku Man City ikishinda 12, mara 10 nyumbani na Liverpool ikishinda 23, mara tano ugenini. Na rekodi za karibuni, katika mechi tano za mwisho, Liverpool imeshinda mbili, sare mbili na Man City imeshinda moja. Hiki ni kipute cha ubabe mwingi.