Man City kuvaana na Liverpool, Arsenal, Chelsea zapewa hawa FA
Muktasari:
- Klabu ya Port Vale imepangiwa kusafiri kwenda London kucheza dhidi ya Chelsea
Droo ya hatua ya robo fainali ya Kombe la FA imefanyika jana usiku, huku vigogo wa soka England wakipata wapinzani wao katika hatua hiyo ambayo itazikutanisha uso kwa uso Manchester City na Liverpool.
Chelsea vs Port Vale
Klabu ya Port Vale imepangiwa kusafiri kwenda London kucheza dhidi ya Chelsea. Klabu hiyo ambayo kwa sasa inashika mkia kwenye msimamo wa League One, iliandika historia ya kufika robo fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1954 baada ya kuitupa nje Sunderland katika hatua ya raundi ya tano.
Vita kali Etihad
Mchezo unaosubiriwa kwa hamu zaidi ni ule utakaopigwa katika Uwanja wa Etihad ambapo Manchester City watamenyana na Liverpool.
Man City wanawania taji lao la nane la FA chini ya kocha Pep Guardiola, huku Liverpool wakitafuta taji baada ya kupoteza nafasi ya ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Southampton vs Arsenal
Mabingwa wa kihistoria wa mashindano hayo Klabu ya Arsenal, imepangiwa kucheza ugenini dhidi ya Southampton, ambao ilifanya maajabu kwa kuiondoa Fulham katika raundi iliyopita.
Kikosi cha Mikel Arteta bado kinawania mataji katika mashindano yote manne wanayoshiriki msimu huu, na ushindi unaweza kuwapeleka Wembley kwa mara ya pili baada ya kufuzu kucheza mechi ya fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Manchester City itakayopigwa Machi 22, 2026.
West Ham vs Leeds
Katika droo nyingine, West Ham itakuwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani kuvaana na Leeds United. West Ham imefuzu kucheza robo fainali baada ya kuitupa nje Brentford jana usiku kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya kutoka sare ya 2-2.
Kwa mujibu wa waandaaji wa mashindano, kila timu itakayofuzu nusu fainali itapata zawadi ya paundi 477,000 (Sh1.7 bilioni) huku ile itakayopoteza katika hatua inayofuata kwenye Uwanja wa Wembley itapewa paundi 530,000 (Sh1.9 bilioni).
Mechi zote za robo fainali zinatarajiwa kuchezwa mwishoni mwa wiki ya Aprili 4 hadi 5.