Man City kiulaini ubingwa

LONDON, ENGLAND.ARSENAL ilitema rasmi ubingwa kwa msimu huu baada ya kukubali kichapo cha mabao 1-0 kutoka kwa Nottinghm Forest wikiendi iliyopita na kuiwezesha Man City kuchukua ubingwa ikiwa sebuleni.

Arsenal ilikuwa ikiongoza kwa muda mrefu kabla ya kupitia kipindi kigumu cha kutopata ushindi kwenye mechi tano kati ya saba hali iliyosababisha Man City ipande kileleni na kutawazwa mabingwa kwa alama 85 baada ya kucheza mechi 35.

Huu unakuwa ni ubingwa wa sita wa Manchester City kwenye EPL huku ikiwa ni ubingwa watatu mfululizo na hiyo imeifanya kuweka rekodi yakuwa tano kufanya hivyo ikiungana na Huddersfield Town, Arsenal, Liverpool na Manchester United.
Mbali ya Arsenal kupoteza ubingwa pia imepoteza kiasi kikubwa cha pesa ambacho ingekipata ikiwa ingekuwa bingwa kwa msimu huu.

Kiasi hicho cha pesa kinatokana na zawadi ya bingwa ambayo msimu uliopita Man City ilipokea Pauni 161 milioni, ambayo ni mjumuisho wa zawadi zote ikiwa pamoja na  pesa ya haki ya matangazo ya televisheni.
Pesa hii huwaganywa kwenye vipengele vitatu kwanza ni ile ya ujumla ambapo kwa msimu uliopita kila timu ilipata Pauni 84 milioni.

Mbali ya hiyo pia hufaidika na pesa za matangazo hayo ya televisheni kulingana na idadi ya mechi zao zilizoonyeshwa kwenye TV ambapo kila mechi zako zinavyozidi kuonyeshwa ndio unavyozidi kuingiza pesa mechi moja inakadiriwa kulipwa Pauni 1.5 milioni.
Mwisho kila nafasi ambayo timu humaliza huwa kuna ongezeko la Pauni 2.5 milioni ambayo pia ni bonasi itokanayo na haki za matangazo ya televisheni.
Hivyo kwa haraka haraka Arsenal imepoteza zaidi ya Pauni 30 milioni ambazo ni zaidi ya bilioni 60 za Kitanzani kwa kushinda kuchukua ubingwa ubingwa huo.

Ukiiondoa Man City katika siku za hivi karibuni timu ambayo imechukua ubingwa huku ikiwa sebuleni ilikuwa ni Leicester City ambayo kwa msimu huu hali yake ni mbaya na inapambana kukwepa kushuka daraja.
Kwa sasa Man City inapambana kuweka rekodi yakuwa timu yapili kwenye historia ya soka nchini England kuchukua mataji matatu kwa mpigo ndani ya msimu mmoja baada ya majirani zao Man United.

Baada ya kupoteza nafasi ya kuchukua taji hilo kocha wa washika mitutu hawa Mikel Arteta amesema hakuna wakulaumiwa zaidi yake na yeye amekubali kuchukua kejeli na kila aina ya neneo baya kwa ajili ya wachezaji wake.

''Nawapongeza Man City kwa kuchukua ubingwa, lakini najisikia vibaya na lazima tukubaliane na ukweli, mechi ya leo (dhidi ya Nottingham), tulitoa goli kirahisi na hatukucheza vizuri kuhakikisha tunarudisha na kushinda, lakini ndio mpira wa miguu pale mnaposhinda mnashangilia na mkipoteza ndio mchezo, hivi karibuni tumekuwa tukitoa mabao kirahisi na hiyo ndio imetumaliza lakini hatuwezi kumlaumu mtu yeyote, tulitakiwa tuwe bora zaidi kwenye siku za mwisho"

"Ni huzuni sana tumefanya kazi kwa miezi 11 tukiwa na lengo la ubingwa na tumekaa kilele ni kwa muda mrefu, tumepambana lakini hatukuwa tunatosha, lazima tujiuguze, nitatafuta njia ya kurudisha motisha kwa wachezaji bado tuna wiki ya kumalizia"
Staili ya Arsenal kuipa ubingwa Man City baada ya kuongoza kwa muda mrefu inafananishwa na kile kilichotokea msimu wa 2013-14 ambapo Liverpool iliipa ubingwa Man City baada ya Steven Gerard kuteleza na kuipa Chelsea nafasi ya kufunga bao.

Msimu wa 1995-96  Newcastle walikuwa na alama 12 mbele ya  Manchester United wakati huo ilibaki michezo 15, lakini ilifanya vibata kwenye mechi nane zilizofuatia ambapo ilishinda mbili tu na hiyo ilisababisha Man United kuwavuka na kuchukua ubingwa.

Arsenal hii iliwahi kutema bungo msimu wa 2007-08 wakati huo wakiwa chini ya Arsene Wenger, walikuwa wanaongoza ligi kwa pointi tano dhidi ya Man United na Chelsea lakini baada ya hapo walipata ushindi wa mechi moja tu kwenye mechi nane na wakamaliza ligi kwenye nafasi ya tatu mbele ya  United na Chelsea.