Mamelodi, Pyramids ngoja tuone itakuwaje

Muktasari:
- Katika mechi za nusu fainali, Mamelodi ilivaana na Al Ahly waliokuwa watetezi na kuwang'oa, huku Pyramids ilivaana na Orlando Pirates ambako Wasauzi waling'oka na kuziacha Pyramids na Mamelodi kukutana leo katika fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kabla ya kurudiana mwezi ujao.
ILE vita ya Wasauzi dhidi ya Wamisri haijaisha wakati leo Jumamosi kule Afrika ya Kusini, jijini Pretoria kwenye dimba la Loftus Versfeld, itapigwa mechi ya mkondo wa kwanza ya fainali ya Ligi ya Mabingwa kati ya wenyeji Mamelodi Sundowns na Pyramids ya Misri.
Katika mechi za nusu fainali, Mamelodi ilivaana na Al Ahly waliokuwa watetezi na kuwang'oa, huku Pyramids ilivaana na Orlando Pirates ambako Wasauzi waling'oka na kuziacha Pyramids na Mamelodi kukutana leo katika fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kabla ya kurudiana mwezi ujao.
Mchezo huo ambao utaanza saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika ya Mashariki utakuwa ni wa tatu kwa timu hizo kukutana katika historia, pia itakuwa ni fainali ya tatu kwa Mamelodi kukutana na timu kutoka Misri.
Mamelodi na Pyramids ambazo ziliwahi kukutana katika mashindano ya msimu uliopita ambapo zilikuwa katika kundi moja (Kundi A), zilimaliza bila kufungana katika mchezo uliopigwa Afrika Kusini kisha ule wa marudiano uliopigwa Misri, Mamelodi ilishinda 1-0.
Hii ni mechi ya tatu ya fainali kiujumla kwa Mamelodi ambayo imewahi kuchukua taji hili mara moja, mwaka 2016 ilipokutana na Zamalek.
Hata hivyo, kabla ya fainali hiyo imewahi kuingia fainali nyingine mwaka 2001 ambapo ilikutana na Al Ahly na kupoteza na raundi hii tena kwenye fainali inakutana na Pyramid ambayo pia inatokea Misri.
Hii ni fainali ya kwanza ya Pyramids tangu kuanzishwa kwake na pia ni msimu wake wa pili kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuwa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho kwa misimu minne.
Mshindi wa matokeo ya jumla katika mechi zote mbili anatarajiwa kupewa zawadi ya Dola 4 milioni (Sh10.7 bilioni), wakati mshindi wa pili akikunja Dola 2 milioni (karibu Sh 5.4 bilioni).
Mechi ya marudiano inatarajiwa kupigwa Juni 1, kwenye dimba la 30 June, jijini Cairo, Misri na itaanza saa 2:00 usiku.
Mwamuzi wa kati wa mechi ya mkondo wa kwanza atakuwa ni Mahmood Ismail kutoka Sudan na ile ya marudiano itasimamiwa Omar Abdulkadir Artan kutoka Somalia.