Mambo sita kubadili upepo Man United

Muktasari:
- Yale maandamano ya zamani yaliyokuwa yakihusisha bendera za rangi ya kijani na dhahabu kumpinga mmiliki Glazer, sasa yamefutwa na mashabiki wametakiwa kuvaa nguo nyeusi kama kwenye maziko siku hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Mashabiki wa Manchester United wametakiwa kubainisha hisia zao bayana wakati wa mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal, uwanjani Old Trafford, Jumapili.
Yale maandamano ya zamani yaliyokuwa yakihusisha bendera za rangi ya kijani na dhahabu kumpinga mmiliki Glazer, sasa yamefutwa na mashabiki wametakiwa kuvaa nguo nyeusi kama kwenye maziko siku hiyo.
Kumaliza hasira hizo za mashabiki wa Man United ili warudi Old Trafford wakiwa na amani ni kitu gani bilionea Sir Jim Ratcliffe na kampuni yake ya Ineos, au familia ya Glazer inapaswa kufanya? Mambo sita haya yakifanyika, yatatuliza hasira za mashabiki wa Man United na kuwa na raha tena na timu yao.
1.Kujenga Old Trafford mpya
Kuanza kazi ya ujenzi wa Old Trafford mpya itaonekana na kila shabiki na kuamini kwamba kuna jambo kubwa linakwenda kutokea kwenye timu yao na dhamira hiyo ipo. Tajiri Ratcliffe ana mpango wa kujenga Old Trafford mpya ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 100,000 wanaoketi ili kubadili sura na mwonekano wa uwanja huo uliojengwa mwaka 1910. Uwanja mpya pia utaongeza mapato, wastani wa Pauni 8 milioni kwa kila mechi, hivyo watakuwa na pesa ya kusajili.
2.Kuboresha mawasiliano
Mashabiki wanahitaji kuona wanahitajika kwenye timu — hivyo mawasiliano mazuri yanapaswa kuimarisha ili kila kinachotokea kwenye timu kifahamike wazi. Ishu ya kupandisha bei ya tiketi, sakata la kupunguza wafanyakazi ni baadhi ya mambo ambayo mashabiki wanahitaji kupewa taarifa mapema.
3.Kuuziwa hisa
Kundi la mashabiki wa Man United — Manchester United Supporters Trust, kwa muda mrefu limekuwa ikizungumzia ishu ya mashabiki kuruhusiwa kuwekeza kwenye timu yao kwa maana ya kupewa nafasi ya kuuziwa hisa. Man United ina mashabiki wengi matajiri, ambao wapo tayari kuingia kwenye mifuko yao kutoa pesa kama Ineos itakuwa na umiliki wa ukakasi wa kitengo cha maendeleo ya michezo kwenye kikosi hicho.
4.Mikakati sahihi
Man United imeweka rekodi kwenye usajili kwa miaka ya hivi karibuni, lakini imenasa wachezaji bila ya kuzingatia ubora wao, kitu ambacho kinamfanya kocha wa sasa Ruben Amorim kuwa na wakati mgumu kutokana na wachezaji hawawezi kumudu staili yake ya uchezaji ya fomesheni ya 3-4-3. Mashabiki wanataka klabu iwe na mipango na mikakati bora kwenye usajili ili kunasa wachezaji wenye faida na wenye kuuzika. Na pia sio kusajili wachezaji ambao wameletwa kwenye timu kwa sababu tu wakala wake na wa kocha ni mmoja.
5.Matokeo mazuri uwanjani
Kuwa na timu inayoshinda, kuwa chini ya kocha mwenye mamlaka, sambamba na mipango ya muda mrefu kwenye maendeleo ya timu hiyo vitaondoa hasira za mashabiki dhidi ya timu yao. Kocha Amorim ametua na matarajio makubwa ambayo bado hayajafikiwa na kuna wasiwasi mkubwa kama Mreno huyo ni mtu sahihi wa kubadili hali ya mambo. Viongozi wanapaswa kukiweka kikosi kwenye utulivu ili kazi ya kocha iwe uwanjani.
6.Familia ya Glazer iondoke jumla
Hitaji kubwa kabisa la mashabiki wa Man United ni kuona familia ya Glazer inaondoka kabisa kwenye timu hiyo. Malalamiko ya mashabiki ni kwamba familia hiyo imekuwa ikitumia tu Man United kama sehemu ya kuvuna pesa, ambapo imeshachukua Pauni 1.3 bilioni kupitia mauzo ya hisa, wakati baba yao alinunua klabu hiyo hata Pauni 800 milioni haifiki mwaka 2005. Na hivi karibuni ilipata Pauni 715 milioni kwa kuuza hisa kidogo kwa tajiri Ratcliffe, huku wao wakiendelea kuwa wamiliki wakuu, wakibaki na hisa asilimia 75.