Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo saba yanayoleta matumaini kwa mashabiki wa Man United

Mambo Pict

Muktasari:

  • Kocha huyo Mreno mwenye umri wa miaka 39, amesema hilo baada ya Man United kuchapwa 3-1 nyumbani Old Trafford na Brighton.

MANCHESTER, ENGLAND: RUBEN Amorim amesema pengine Manchester United hii ni mbovu zaidi kuwahi kutokea kwenye historia ya klabu hiyo.

Kocha huyo Mreno mwenye umri wa miaka 39, amesema hilo baada ya Man United kuchapwa 3-1 nyumbani Old Trafford na Brighton.

Baada ya kipigo hicho, ambacho kilikuwa cha sita kwa Man United katika mechi 12 ilizocheza nyumbani kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England na cha 10 katika ligi msimu huu, Amorim alisema: “Tumekuwa timu mbovu zaidi kwenye historia ya Manchester United.

“Najua mnataka vichwa vya habari, lakini nasema hivyo kwa sababu nafahamu tunahitaji kuibadilisha hii hali. Haya nendeni, kichwa chenu cha habari hicho.”

Maneno hayo ya Amorim yamekuja wiki mbili baada ya kukiri kwamba ishu ya timu hiyo kupambana kujinasua kwenye janga la kushuka daraja linawahusu.

Kwa hilo, mambo yanaonekana kuwa magumu kwa mashabiki wa Man United, lakini shaka isiwe juu yao kutokana na mambo haya saba yenye matumaini.


Moja: Amad Diallo

Winga huyo Muivory Coast hakuna ubishi ni mmoja wa wachezaji wa Man United wanaocheza kwa viwango bora msimu huu. Kiwango chake tangu Amorim alijiunga na timu hiyo kimekuwa kikiongezeka kila siku tofauti na alivyokuwa chini ya kocha Erik ten Hag, ambapo alikuwa hapewi nafasi ya kucheza.

Mabao muhimu kwenye mechi dhidi ya Manchester City na Liverpool, sambamba na ile hat-trick yake ya Alhamisi iliyopita dhidi ya Southampton, imeonyesha matumaini makubwa kwa Man United kwamba itakuwa salama kwenye mikono ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22.


Mbili: Old Trafford mpya

Uwanja wa Old Trafford umeshazeeka, zama zake zimeshakwisha. Ni uwanja uliopitwa na wakati, unawapa matatizo mengi mashabiki ikiwamo panya kuwa wengi na paa lake kuvuja. Lakini, wasiwasi uwekwe kando, mabadiliko makubwa yanakuja kwenye uwanja huo.

Kikosi kazi kimeundwa na mmiliki mpya, bilionea Sir Jim Ratcliffe kikifanya mchakato wa upembuzi yakinifu ili kupata uamuzi mmoja kama kujenga uwanja mpya kabisa au kuuboresha huo ili kuwa wa kisasa.

Mpango ni kutumia Pauni 2 bilioni kuifanya Old Trafford kuwa mpya, ambapo inatazamiwa kuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 100,000 wanaoketi.


Tatu: Matumaini ya Ligi ya Mabingwa Ulaya

Man United kwa sasa inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, pointi 12 nyuma ya timu inayoshika nafasi ya nne, ambao ni mahasimu wao, Manchester City.

Lakini, matumaini ni makubwa kwamba Man United bado ina nafasi ya kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Hii ni kwa sababu timu hiyo inapewa nafasi kubwa ya kushinda ubingwa wa Europa League, sambamba na Tottenham, ambayo kwenye msimamo wa Ligi Kuu England inashika nafasi ya 15.

Kwa Man United kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, tiketi hiyo wanapaswa kuisaka kwa kushinda Europa League.


Nne: Kucheza vizuri mechi kubwa

Man United imeshindwa kuzifunga Ipswich, Wolves, West Ham, Crystal Palace na Tottenham msimu huu. Lakini, imeonyesha kiwango kizuri sana kwenye mechi dhidi ya timu kubwa, jambo ambalo linatoa uhakika wa kwenda kufanya vizuri kwenye Europa League itakapokwenda kuchuana na timu kubwa.

Man United imeitupa nje Arsenal kwenye Kombe la FA tena uwanjani Emirates na ilinyakua pointi muhimu kabisa kwenye mechi dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield na kuichapa Man City uwanjani Etihad kwenye mechi za Ligi Kuu England.


Tano: Kuondoa mizigo kikosini

Man United imetumia pesa nyingi sana kwa miaka ya hivi karibuni, kuanzia kwenye kumpa Marcus Rashford dili la Pauni 325,000 kwa wiki na kutoa Pauni 85.5 milioni kunasa saini ya Antony.

Baada ya sasa kuwa chini ya bilionea Ratcliffe moja ya mambo ambayo Man United inafanya ni kujaribu kuondoa wachezaji ambao mchango wao hauendani na viwango wanavyolipwa.

Kinachoripotiwa kwa sasa ni kwamba Antony anakaribia kuondoka kwa mkopo na kitu kama hicho kinaweza kumhusu Rashford pia kabla ya dirisha hili la Januari kufungwa ili kikosi kuwa na nafasi ya kuleta wachezaji wengine wenye maana.


Sita: Kushikilia msingi mkuu

Kwa mashabiki wa Man United ambao walikuwa wamepaniki juu ya usimamizi wa kikosi hicho kwa benchi la ufundi lililopita kwa sasa wanahamasika na uwepo wa Ruben Amorim, ambaye amekuwa akisisitiza ataendelea kushikilia msingi wake mkuu wa fomesheni inayopaswa kutumika na wachezaji wa Man United bila ya kujali kwamba wachezaji watapata shida hadi kuzoea mfumo huo.

Chini ya Erik ten Hag, Man United haikuwa ikifahamika inacheza mtindo gani na sasa ujio wa Amorim umeonyesha kile ambacho timu itakuwa inacheza ili kuwa na utambulisho wake wa kueleweka.


Saba: Msaada kutoka kwa gwiji wao

Wasiwasi wa Amorim ni kama kikosi chake kuingia kwenye wimbi la kuwa moja ya timu zitakazokuwa kwenye vita kali ya kujinasua na janga la kushuka daraja.

Lakini, katika vita hiyo Man United inaweza kusaidiwa na straika wao wa zamani, Ruud van Nistelrooy, ambaye kwa sasa ni kocha wa Leicester City.

Kabla ya kutua huko King Power, Mdachi huyo alikuwa kocha wa mpito Man United.

Na sasa Leicester City ikiwa imepoteza mechi saba mfululizo chini ya Van Nistelrooy linaifanya Man United kutokuwa na wasiwasi wa kudumbukia kwenye shimo la kushuka daraja kwa sasa, watakuwa na muda wa kujipanga.