Malipo ya siri yaiponza Chelsea yafungiwa mwaka mmoja
Muktasari:
- Malipo haya yaligunduliwa wakati wa uchunguzi (due diligence) baada ya umiliki mpya wa Marekani kununua klabu hiyo 2022 na wamiliki hao waliripoti wenyewe ukiukaji huo kwa Ligi Kuu, FA na UEFA.
LIGI Kuu England imekamilisha uchunguzi juu ya malipo ya siri yaliyofanywa na Chelsea kati ya 2011 na 2018 wakati Roman Abramovich alipokuwa mmiliki wa klabu hiyo yenye maskani yake London.
Malipo haya yaligunduliwa wakati wa uchunguzi (due diligence) baada ya umiliki mpya wa Marekani kununua klabu hiyo 2022 na wamiliki hao waliripoti wenyewe ukiukaji huo kwa Ligi Kuu, FA na UEFA.
Chelsea imepigwa faini kubwa zaidi katika historia ya ligi hiyo pauni 10.75m. Pamoja na faini hiyo, klabu hiyo imefungiwa mwaka mmoja kusajili lakini hukumu hiyo ni ndani ya miaka miwili.
Faini hiyo inahusiana na malipo ya siri kwa mawakala yenye thamani ya pauni 47.5m na ukiukaji wa kanuni kuhusu usajili wa wachezaji vijana.
Uchunguzi umebaini kuwa malipo hayo yalifanywa kwa idhini ya wafanyakazi wa ngazi ya juu na wakurugenzi wa zamani. Taarifa rasmi ya Ligi Kuu ilieleza kuwa malipo hayo yalitolewa bila kuorodheshwa kwenye hesabu rasmi za klabu zilizowasilishwa kwa mamlaka husika kwa wakati huo.
Mbali na hiyo, Chelsea pia imepigwa marufuku kusajili wachezaji wa akademi kwa miezi tisa ambayo imeanza mara moja. Marufuku hii inahusiana na ukiukaji unaohusiana na wachezaji waliokuwa katika akademi kati ya 2019 na 2022.
Ripoti ya Ligi Kuu pia ilitaja baadhi ya mabadiliko ya wachezaji yanayohusiana na malipo haya, yakiwemo Eden Hazard, Samuel Eto'o, Willian, Ramires, David Luiz, Andre Schurrle na Nemanja Matic.
Hata hivyo, ripoti hiyo haikuonyesha kuwa wachezaji hao walikuwa na hatia yoyote na majina ya wachezaji wanne yamefichwa.
Faini ya jumla ya pauni 20milioni ilipunguzwa nusu kwa sababu Chelsea walijiripoti wenyewe na kushirikiana kikamilifu na uchunguzi.
Ligi Kuu ilieleza kuwa kuripoti mapema na kushirikiana kulikuwa sababu muhimu za kupunguza adhabu, ikionyesha kuwa klabu imewajibikaji.
Adhabu hiyo inaweza kuanza mara moja ikiwa Chelsea watakiri makosa mengine ya aina hiyo. Hali hii inatoa nafasi kwa klabu kuendelea na shughuli zake za usajili kwa sasa, mradi tu isirudie makosa hayo.
Kocha wa sasa wa Chelsea, Liam Rosenior, alisema kuwa jambo hili haliwezi kuwa kikwazo kwa klabu hiyo. Aliongeza kuwa klabu inapaswa kuendelea kupanga mikakati yake ya muda mrefu ili kuimarisha kikosi.
Chelsea ilipigwa pia faini ya pauni 8.64milioni na UEFA mwaka 2023 kutokana na ripoti zisizo kamili za kifedha kutoka kwa wamiliki wa zamani mwaka 2018 na 2019. Uchunguzi huo ulibaini malipo kadhaa yaliyoelekezwa kwenye kampuni za offshore ambazo hazikuwa kwenye hesabu rasmi za klabu.