Makhachev amtwanga Maddalena na kubeba taji jingine la UFC
Muktasari:
- Mbabe huyo alitwaa taji hilo kwenye Ukumbi wa Madison Square Garden, usiku wa kuamkia leo Jumapili, huku Valentina Shevchenko alitetea taji lake la uzito wa fly katika pambano jingine kubwa lililopigwa ukumbini hapo.
NEW YORK, MAREKANI: ISLAM Makhachev, mpiganaji wa mchanganyiko wa sanaa za mapigano (MMA) amefanya kweli baada ya kumzidi ujanja Jack Della Maddalena katika pambano la raundi tano na kutwaa ubingwa wa UFC uzito wa welter.
Mbabe huyo alitwaa taji hilo kwenye Ukumbi wa Madison Square Garden, usiku wa kuamkia leo Jumapili, huku Valentina Shevchenko alitetea taji lake la uzito wa fly katika pambano jingine kubwa lililopigwa ukumbini hapo.
Makhachev mwenye rekodi ya 28-1 hakuona ugumu kupanda daraja la uzito baada ya kuachia taji la lightweight ili kutafuta changamoto mpya, kwani alimtawala kabisa mpinzani huyo kutoka Australia kwa dakika 25 kupitia mbinu za mieleka na kufikisha ushindi wa 16 mfululizo UFC.
Mwanamieleka huyo mwenye umri wa miaka 34 alianza kwa kumdhoofisha mpinzani mwenye umri wa miaka 29 kwa mateke ya sehemu ya mguu (calf kicks), kisha kuzindua mashambulizi ya kudumu ya mieleka.
Della Maddalena hakuwa na jibu kwani kuna wakati alinaswa chini akipambana na vitisho vya kumlazimisha kujisalimisha chini ya shinikizo kubwa kwa muda mrefu.
“Huu ndio mpango wangu. Sio siri, wapinzani wangu wote wanaujua, na hakuna anayeweza kuuzuia,” Makhachev alisema kabla ya kutaja anataka kutetea taji lake kwa mara ya kwanza kwenye tukio linalopendekezwa kufanyika kwenye Uwanja wa Ikulu ya White House mwakani.
Majaji wote watatu walimpa alama ya 50-45 na kumfanya Makhachev kuwa mpiganaji wa 11 katika historia ya UFC kushika mataji katika madaraja mawili tofauti ya uzito.
Katika pambano la pili kwa ukubwa, ndoto ya Zhang Weili kujiunga na kundi hilo haikutimia baada ya Shevchenko mwenye ujanja mwingi kumzidi kwa pointi na kutoa onyesho jingine thabiti akitetea taji la uzito wa flyweight.
Mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 37 kutoka Kyrgyzstan alionyesha uwezo kamilikwa kuumpiga mpinzani wake kutoka China kwa makonde ya mbali, kumuumiza kwa mateke makali ya mwilini na kumuangusha chini wakati wowote alipojisikia kuwa katika hatari na kushinda raundi zote tano kwa maoni ya majaji na hivyo kubaki bingwa.
“Niliandaa pambano hili kana kwamba ni changamoto ngumu zaidi maishani mwangu,” Shevchenko alisema ulingoni baada ya kufanya dansi yake ya ushindi kama kawaida; “Hivi ndivyo ninavyokiita sanaa ya mapigano. Wanapokabiliwa nami hapa, hawawezi kufanya chochote.”