Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MAYWEATHER VS PACQUIAO: Miaka 10 tangu pambano la karne!

Muktasari:

  • Imepita miaka 10 tangu kile kilichokuwa pambano lenye faida na bora zaidi katika historia ya ngumi kufanyika.

LAS VEGAS, MAREKANI: ACHANA na lile pambano la ‘The Rumble in the Jungle’ lililopigwa Oktoba 30, 1974 nchini Zaire (sasa DR Congo) kati ya Muhammad Ali dhidi ya George Foreman ambalo ndilo linalotajwa kuwa bora la muda wote ulingoni, lakini Mei 2, 2015 pambano lililosubiriwa kwa hamu kwa miaka kadhaa hatimaye lilifanyika na hadi leo linabaki kuwa lenye faida kubwa zaidi katika historia ya ngumi kwenye miaka ya 2000. Hili lilikuwa ni pambano bora kabisa la karne la 21.

Imepita miaka 10 tangu kile kilichokuwa pambano lenye faida na bora zaidi katika historia ya ngumi kufanyika.

Kabla ya pambano hilo Mayeweather alikuwa na rekodi ya kupigana mara 47 bila kupoteza, huku akishinda mara 26 kwa knockout ilhali Pac-man alikuwa amepigana mapambano 57, sare tano na vipigo viwili, lakini akiwalambisha mchanga wapinzani wake mara 38 kwa knockout.

Hadi leo, pambano kati ya Floyd Mayweather na Manny Pacquiao linashikilia rekodi ya mauzo ya runinga Marekani upande wa  pay-per-view (PPV), yaani malipo kwa kutazama tukio kwa mashabiki wanaokuwa majumbani, likifikia milioni 4.6 kupitia televisheni maarufu za michezo HBO na Showtime.

Pambano hilo lililoitwa ‘Fight of the Century’ lilikuwa na mafanikio makubwa kiasi cha kuingiza mapato ya Dola 600 milioni pamoja na malipo ya PPV kwani watu walilipia kati ya Dola 90 hadi 100 kwa HD kuangalia tu wababe hao wakizichapa.

Sehemu kubwa ya fedha hizo ziliingia kwenye mfuko wa Mayweather ambaye alikuwa ni promota wake mwenyewe. Nchini Ufilipino, hata shughuli za Bunge la nchi ziliahirishwa kwa siku kadhaa kwani wabunge wengi walisafiri kwenda Marekani kushuhudia pambano hilo moja kwa moja. Ikumbukwe kwamba Pacquiao maarufu kama Pac-Man ni raia wa nchi hiyo.

Pambano lilifanyika katika ukumbi wa MGM Grand Garden Arena mjini Las Vegas, Marekani na Mayweather ambaye ni Mmarekani ndiye aliyeshinda.

Mmarekani huyo ambaye alidhibiti ngumi za umbali vizuri alimshinda Pac-Man kwa uamuzi wa pamoja wa majaji (116–112, 116–112 na 118–110). Mabondia wote wawili waliingia ulingoni wakiwa mabingwa wa uzani wa welter ambapo Mayweather akiwa na miaka 38 na Pacquiao miaka 36.

Ukweli ni kwamba pambano hilo halikufanyika hadi pale Pretty Boy (jina la utani la Floyd) alipolitaka. Pac-Man alikuwa ameshinda mapambano matatu mfululizo baada ya kupoteza pambano lake la nne dhidi ya Juan Manuel Marquez, aliyemshinda kwa knockout iliyobaki kwenye kumbukumbu za historia.

Kama pambano hilo lingefanyika 2009 wakati mazungumzo ya awali yalipoanza, huenda lingekuwa la kusisimua zaidi kuliko lilivyokuwa hatimaye katika ulingo wa MGM mnamo Mei 2, 2015. Bila shaka wawili hao walikuwa mabondia bora zaidi wa ‘pound-for-pound’ wa wakati huo na ilikuwa ni Mayweather aliyeanza kumzungumzia Pacquiao, lakini alikataa mapato kugawanywa sawa kwa 50/50.

Katika pambano hilo umaarufu wa Mayweather na ubora aliokuwa nao ulimfanya akunje Dola 180 milioni, huku Pac-man akiweka kibindoni Dola 120 milioni. Mkwanja huo ndio uliokuwa mkubwa zaidi kuwahi kulipwa kwa mabondia katika ulimwengu wa masumbwi na kwa hakika haijawahi kufikiwa rekodi hiyo hadi sasa.

Pac-Man alikuwa amefungwa kimkataba na Top Rank chini ya promota wa zamani wa Mayweather aitwaye Bob Arum ambaye pia hakukubali masharti hayo.

Mwaka 2010 ulikuwa mwaka wa tuhuma nzito kutoka kwa Floyd dhidi ya Pac-Man, ambapo alisema kuwa kama mpinzani wake angekubali kipimo cha damu siku 30 kabla ya pambano, basi lingefanyika. Pacquiao alidai angefungua kesi ya kashfa dhidi ya Mayweather kwa kumtuhumu kutumia dawa za kuongeza nguvu (doping).

Bondia huyo aliongeza kuwa angeweza kufanyiwa vipimo kadhaa vya damu katika miezi ya maandalizi, lakini si ndani ya siku 30 kabla ya pambano kwa sababu aliamini ingemweka katika hali ya udhaifu. Mazungumzo yaliendelea kugonga mwamba, na mwaka 2012 baada ya Marquez kumpiga KO mazungumzo yakafa tena.

Mwaka 2014, Pacquiao aliporejea kuwa bingwa mazungumzo yakafufuliwa. Mitandao ya kijamii ilijaa mijadala na kufikia Januari 2015, Bob Arum alikubaliana na timu ya Money (Mayweather) kuhusu masharti yote.

Kilichobaki ilikuwa ni mabondia wenyewe kutia saini. Walikutana uso kwa uso Miami wakati wa mechi ya NBA ya Miami Heat katika mkutano ambao haukupangwa, lakini ulitikisa ulimwengu wa ngumi.

Pac-Man alikuwa Miami kama jaji wa shindano la Miss Universe Januari 25, lakini ndege yake ya kurejea Ufilipino iliahirishwa kutokana na hali mbaya ya hewa, hivyo akaamua kwenda kutazama mechi ya Heat. Baada ya mazungumzo mafupi ukumbini walikubaliana kukutana usiku huo hotelini alikofikia Pacquiao ili kujadili baadhi ya vipengele.

Hapo ndipo walipozungumzia kuhusu vipimo vya dawa, nani angeingia ulingoni wa mwisho na ni jina lipi lingewekwa mwanzo kwenye mabango. Mayweather alimpigia simu mkuu wa Showtime Sports kumwambia kila kitu kimekamilika, na HBO na Showtime wakakubaliana namna ya kufanikisha pambano hilo.

Baada ya maandalizi yote, ilitangazwa kwamba ili mtu aketi mstari wa mbele katika ukumbi wa MGM angelazimika kulipa Dola 180,000 na vifurushi vya kifahari vilitolewa kwa wageni wa hadhi ya juu pekee.

Miongoni mwa waliokuwepo walikuwa Prince, Robert De Niro, Clint Eastwood, Jay Z na Beyonce, Denzel Washington, Jake Gyllenhaal, Bradley Cooper, Christian Bale na Ben Affleck.

Kutoka ulimwengu wa michezo walikuwepo mastaa wa kikapu wa zamani kina Magic Johnson na Michael Jordan ilhali soka la Kimarekani liliwakilishwa vyema na Tom Brady na Charles Barkley, huku tenisi ikiwakilishwa na Andre Agassi na Steffi Graf. Hata Donald Trump na Melania walihudhuria.

Ikumbukwe kwamba Trump alikuwa promota maarufu wa ngumi za kulipwa Marekani na ndiko alikovunia utajiri alionao sasa. Trump aliwahi kuwa promota na meneja na promota wa bondia maarufu wa zamani Mike Tyson.

Kwa sasa wakiwa wameshastaafu mabondia hao ndio tajiri zaidi pengine kuliko wote duniani, Pac-man akiwa na mkwanja unaofikia Dola 220 milioni, ingawa wakati anazichapa alikuwa na Dola 553 milioni ilhali Mayweather ana ukwasi wa Dola 500 milioni kwa sasa, lakini wakati wake akiwa ulingoni ulifikia Dola 1.2 bilioni.

Kwa hakika pambano la Pac-man lilikuwa ni tukio ambalo hakuna mtu aliyependa kulikosa kipindi hicho na ni ni bahati mbaya tu kwamba halikufanyika miaka mitano mapema. Oktoba 29, mwaka huu, Pac-man alizungumzia dhamira ya kurudia na Mayweather kwani hakuridhishwa na matukio ya miaka 10 iliyopita. Tusubiri tuone iwapo kambi ya Mayweather itaku-baliana na ombi hilo.