Liverpool haishikili EPL, yaweka rekodi hii
Muktasari:
- Liverpool ilikuwa ya kwanza kufumania nyavu kupitia staa wao Ryan Gravenberch dakika ya 10 ambaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo (miaka 23) zaidi kufunga na kutoa asisti katika mechi ya dabi dhidi ya Everton.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL imeendelea kugawa dozi katika Ligi Kuu England ikifanikiwa kushinda mchezo wa tano mfululizo msimu huu baada ya kuifunga Everton mabao 2-1 katika dabi ya Jiji la Liverpool na kuweka rekodi.
Hii inakuwa ni mara ya tano kwao kushinda mechi tano mfululizo za mwanzo katika Ligi Kuu England tangu msimu 1979/1978 na kati ya mara hizo tano, msimu wa 2019/20 ilimaliza ikiwa bingwa.
Ushindi huo umewawezesha kufikisha pointi 15 ikiendelea kusalia katika kilele cha msimamo wa ligi na haitoshuka hata Arsenal kesho Jumapili ikishinda dhidi ya Manchestee City.
Liverpool ilikuwa ya kwanza kufumania nyavu kupitia staa wao Ryan Gravenberch dakika ya 10 ambaye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo (miaka 23) zaidi kufunga na kutoa asisti katika mechi ya dabi dhidi ya Everton.
Liverpool ambayo ilionekana kuitawala zaidi mechi ilijipatia bao la pili lililofungwa na mshambuliaji Hugo Ekitike dakika 29.
Everton iliamka katika kipindi cha pili na ikapata bao la kufutia machozi kupitia Idrissa Gueye ambaye baada ya bao hilo amekuwa mchezaji wa pili wa Everton mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kufunga bao katika mechi ya dabi ya Merseyside. Gueye ana umri wa miaka 35 na siku 359.
Anayeshikilia namba moja katika rekodi hiyo kwa sasa ni Sam Chedzdoy aliyefunga akiwa na miaka 37, Februari 1926.
Baada ya mechi hiyo, Everton sasa inashika nafasi ya nane ikiwa na pointi saba ilizopata kwa kushinda mechi mbili, sare moja na kufungwa mbili.