Mahakama Hispania yafunga uchunguzi kifo cha Diogo Jota na mdogo wake
Muktasari:
- Ndugu hao walipoteza maisha Julai 3, 2025 kaskazini mwa Hispania, baada ya gari lao aina ya Lamborghini kutoka nje ya barabara kuu ya A-52 karibu na eneo la Cernadilla.
ZAMORA, HISPANIA: MAHAKAMA nchini Hispania, imeamua kuwa hakukuwa na kosa la jinai katika ajali ya gari iliyosababisha kifo cha mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, Diogo Jota na mdogo wake, Andre Silva.
Ndugu hao walipoteza maisha Julai 3, 2025 kaskazini mwa Hispania, baada ya gari lao aina ya Lamborghini kutoka nje ya barabara kuu ya A-52 karibu na eneo la Cernadilla.
Kwa mujibu wa uchunguzi rasmi, ajali hiyo ilisababishwa na tairi la gari kupasuka wakati Jota alipokuwa akijaribu kulipita gari lingine. Gari hilo lilipoteza mwelekeo, likagonga kizuizi cha barabarani, kisha kushika moto.
Mahakama Kuu ya Zamora, iliyopo kaskazini-magharibi mwa Hispania, ilisema baada ya kupitia ushahidi wote pamoja na ripoti za wataalamu wa ajali za barabarani, hakuna hatua za jinai zinazohitajika kuchukuliwa.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa uamuzi huo hauzuii familia au wahusika wengine kufungua kesi ya madai ya kiraia iwapo wataona inafaa.
Wakati wa ajali hiyo, Jota na ndugu yake walikuwa safarini kuelekea mji wa bandari wa Santander ili wapande kivuko kuelekea Uingereza, ambako Jota alitarajiwa kujiunga na Liverpool kwa maandalizi ya msimu mpya.
Inaelezwa kuwa, Jota ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo baada ya kushauriwa na madaktari kuepuka kusafiri kwa ndege kufuatia kufanyiwa upasuaji wa mapafu mapema kipindi hicho.
Tukio hilo lilitokea siku 11 baada ya Jota kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Rute Cardoso, jijini Porto, Ureno.
Mazishi ya ndugu hao yalifanyika siku mbili baada ya vifo vyao katika mji wa Gondomar karibu na Porto, ambako wote walikulia kisoka.
Wachezaji wa Liverpool walihudhuria mazishi hayo huku nahodha Virgil van Dijk akibeba shada la maua lililoundwa kama jezi yenye namba 20 ya Jota.
Naye Andrew Robertson alibeba shada lenye namba 30, namba aliyokuwa akivaa Andre Silva.
Silva naye alikuwa mchezaji wa kulipwa, akiichezea FC Penafiel nchini Ureno baada ya kukulia katika akademi ya Porto.