Maguire mambo magumu Man United
Muktasari:
- Beki huyo wa kati amekuwa akitoa kiwango bora kabisa katika maisha yake akiwa Manchester United, wakati hatma yake katika klabu hiyo ikiwa bado haijaamuliwa. Mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu huu na bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa ya kuongeza muda.
MANCHESTER, ENGLAND: MUSTAKABALI wa beki Harry Maguire katika kikosi cha Manchester United bado haujulikani, huku ikiwa imebaki miezi michache kabla ya mkataba kwisha.
Beki huyo wa kati amekuwa akitoa kiwango bora kabisa katika maisha yake akiwa Manchester United, wakati hatma yake katika klabu hiyo ikiwa bado haijaamuliwa. Mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu huu na bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa ya kuongeza muda.
Inaripotiwa kuwa Maguire anataka kubaki Manchester, na amerejea katika kikosi cha kwanza chini ya kocha wa muda Michael Carrick. Tangu arejee kikosini, amepoteza mchezo mmoja tu katika mechi nane alizoanza Ligi Kuu England.
Ikiwa imebaki chini ya miezi mitatu kabla ya msimu kumalizika huku United ikipambana kutafuta nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa, kuna mjadala mkubwa kuhusu mustakabali wa beki huyo.
Katika msimu wake wa saba Old Trafford, miezi miwili iliyopita ilionekana kana kwamba maisha ya soka ya Maguire Manchester yalikuwa yanaelekea mwisho, chini ya kocha Ruben Amorim ambapo alikuwa ameanza mechi nne tu za ligi.
Hata hivyo, ujio wa Carrick umefufua upya kiwango cha mchezaji huyo wa timu ya taifa ya England ambaye amechangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa United katika msimamo wa ligi.
Ingawa bado haijaamuliwa kama Maguire, mwenye miaka 33, atapewa mkataba mpya, The i Paper inaripoti kuwa klabu inafikiria kumpa mkataba mpya, lakini kwa mshahara pungufu. Pendekezo hilo linataka mshahara wake wa sasa wa Pauni 190,000 kwa wiki upunguzwe hadi takriban Pauni 100,000 kwa wiki.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa Maguire yupo tayari kufikiria masharti hayo mapya. Akiwa miongoni mwa mataa waliodumu muda mrefu zaidi katika kikosi cha United na nahodha wa zamani wa timu, Maguire anaheshimiwa sana na wachezaji wenzake ambao wanataka klabu imuongezee mkataba.
Kwa mujibu wa The Sun, wachezaji wengi ndani ya kikosi wanaamini itakuwa kosa kubwa kama Maguire hatapewa mkataba mpya kutokana na kiwango na mchango wake katika kuwasaidia wachezaji chipukizi kikosini.