Madueke: Muda wa mataji umefika
Muktasari:
- Winga huyo Mwingereza alikamilisha uhamisho wake wa Pauni 52 milioni kutoka Chelsea - na Arsenal itatanguliza kulipa Pauni 48 milioni, kisha itamalizia Pauni 4 milioni, kulingana na viwango vya mchezaji huyo uwanjani.
LONDON, ENGLAND: STAA Noni Madueke amekamilisha dili lake la kujiunga na Arsenal na hakutaka kuchukua muda kuwaambia mashabiki wa timu hiyo: “Sasa ni muda wa mataji.”
Winga huyo Mwingereza alikamilisha uhamisho wake wa Pauni 52 milioni kutoka Chelsea - na Arsenal itatanguliza kulipa Pauni 48 milioni, kisha itamalizia Pauni 4 milioni, kulingana na viwango vya mchezaji huyo uwanjani.
Amesaini dili refu la kukipiga Emirates hadi 2030.
Madueke ni usajili wa nne kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya Kepa, Martin Zubimendi na Christian Norgaard. Beki wa Valencia, Christhian Mosquera na straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres wapo kwenye mchakato wa kukamilisha dili zao za uhamisho ili kutua kwenye kikosi hicho cha Kocha Mikel Arteta.
Akizungumzia juu ya msimu ujao, Madueke alisema: “Kushinda mataji yote tutakayoshindania ni kitu ambacho nina uhakika tunaweza kukifanya. Na kingine ni kuisaidia timu katika kila hali ninayoweza kama mchezaji, lakini pia kama mtu.”€
Katika kuhakikisha anawahi kukamilisha dili lake la kujiunga na Arsenal, Madueke aliondoka kwenye kikosi cha Chelsea kabla ya hata mechi ya fainali ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Paris Saint-Germain, ambapo The Blues ilishinda 3-0.
Mkurugenzi wa michezo wa Arsenal, Andrea Berta alisema: “Tumefarijika kwa kukamilisha dili hili la mchezaji kijana mwenye kipaji kikubwa Noni Madueke. Namba za Noni za msimu wa karibu zinajieleza, ni mchezaji mwenye ujuzi mkubwa, atakuja kuongeza kitu kikubwa kwenye kikosi chetu.”
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alisema: “Tunafurahia kumkaribisha Noni Madueke kwenye kikosi. Noni ni kijana wa aina yake kutokana na kiwango chake na namba zake za misimu ya karibuni. Ni mmoja wa washambuliaji wa pembeni wenye vipaji vikubwa kwenye Ligi Kuu England.”