Madrid 2 Atletico 1... Watoto wa Man City wasimamia shoo

Muktasari:
- Los Blancos imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua inayofuata baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi hiyo. Rodrygo aliitanguliza Real Madrid kiufundi kabisa kwenye dakika ya nne ya mchezo.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imesherehekea mechi ya 500 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi mbele ya mahasimu wao wa jiji la Madrid, Atletico kwenye kipute cha hatua ya 16 bora.
Los Blancos imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua inayofuata baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi hiyo. Rodrygo aliitanguliza Real Madrid kiufundi kabisa kwenye dakika ya nne ya mchezo.
Lakini, wakati ikionekana kama kikosi hicho cha Carlo Ancelotti kimemaliza mambo katika mechi hiyo, mkali wa zamani wa Manchester City, Julian Alvarez, aliirudisha Atletico mchezoni kwa kufunga bao maridadi.
Fowadi huyo Muargentina alilifuta bao hilo la Mbrazili kwenye dakika 32 na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1. Alvarez alifunga bao lake kifundi sana.
Kipindi cha pili, Atletico ilianza kutawala mchezo na kuonekana kama itatia mchanga kwenye sherehe za mechi ya 500 za Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku huo.
Lakini, alikuwa mchezaji mwingine wa zamani wa Man City, Brahim Diaz aliyeamua matokeo ya mwisho ya mchezo huo, baada ya kuwavuruga mabeki wa Atletico na kuweka mpira nyavuni, akimchambua kipa Jan Oblak kwa shuti la chinichini kwenye dakika ya 55.
Mabao hayo mawili bila ya shaka yatamfanya kocha Pep Guardiola ajikune kichwa huko alipo baada ya kuwaachia wachezaji hao kuondoka na sasa wanatamba na timu nyingine kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Man City ilitupwa nje ya michuano hiyo na Real Madrid kwenye mechi ya mchujo, huku mmoja wa wachezaji aliyewafanyia jambo baya ni Diaz, walipocheza uwanjani Etihad.
Man City ya msimu huu imekosa kabisa makali, imeshindwa kutetea taji lake la Ligi Kuu England na imetupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Ligi. Taji pekee ililobakiza yenye uwezo wa kulibeba kwa msimu huu ni Kombe la FA. Na mashabiki walitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kuzungumzia hilo.
Shabiki wa kwanza aliposti: "Hutaelewa kwanini Man City ilimuuza."
Na mwingine alisema: "Lawama kwa Pep kwa kugoma kumchezesha na Erling Haaland."
Real Madrid inaamini kwamba uongozi wao huo wa tofauti ya bao moja utawabeba kwenye vita yao ya mtoano mbele ya Atletico Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.