Macheda amfunda Kobbie Mainoo

MANCHESTER, ENGLAND. FEDERICO Macheda amemwambia Kobbie Mainoo asirudie makosa ambayo yeye aliyafanya ya ‘kuvimba kichwa’ baada ya kupata umaarufu mkubwa akiwa na umri mdogo pale Old Trafford.

Macheda alisema hilo baada ya Mainoo naye kufunga bao dhidi ya Liverpool, ambalo linafanana kabisa na lile alilofunga yeye kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Aston Villa, Aprili 2009.

Kipindi hicho, akiwa na umri wa miaka 17, Macheda alifunga bao maridadi kabisa dhidi ya Aston Villa, ambalo kwa staili aliyofunga ilionekana kurudiwa na Mainoo kwenye sare ya 2-2 na Liverpool uwanjani Old Trafford.

Kwa sasa akichezea timu ya chini ya Ankaragucu ya huko Uturuki, Macheda alikiri mafanikio kumpanda kichwani.

Alisema: “Baada ya lile bao nilidhani nimemaliza maisha. Sikujua nini kitakuja mbele. Nilidhani nitabaki kwenye kiwango kilekile badala ya kupambana kuongeza kiwango. Nilikuwa mkubwa kwa ghafla tu.

“Nilikuwa mdogo, hivyo sikuliangalia hilo kwa ukubwa wake. Lakini, kumbe ningeweza kufanya zaidi na zaidi. Kwa namna Mainoo anavyocheza, atakwenda kuwa mgumu sana katika kipindi cha miaka 10. Lakini, anachopaswa apambane asilewe sifa sasa hivi.”

Macheda alisema baada ya bao lake, alikuwa kwenye kinywa cha kila mtu kabla ya kupata majeraha, ambayo baadaye yalimfanya apoteze kiwango chake na kushindwa kupata nafasi ya kucheza.

Hata hivyo, Macheda anadhani kwenye kikosi cha Man United kwa sasa ni rahisi sana kupata namba ya kucheza.

Alisema: Kipindi changu ilikuwa ngumu kuwa sehemu ya timu ya Man United, hata mazoezini. Safu ya ushambuliaji ilikuwa na wachezaji wa viwango vya dunia, Tevez, Ronaldo, Rooney na Berbatov. Siku hizi ni rahisi sana.

“Kobbie ana kipaji kikubwa, anaweza kutoboa.”