Mabosi Juventus wajitosa dili la Silva
Muktasari:
- Hata hivyo, Silva mwenye umri wa miaka 31, huduma yake pia inahitajika na vigogo wengine barani Ulaya ikiwa ni pamoja na Galatasaray ya Uturuki na Inter Miami ya Marekani.
JUVENTUS imeanza mazungumzo na wawakilishi wa kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Ureno, Bernardo Silva ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Hata hivyo, Silva mwenye umri wa miaka 31, huduma yake pia inahitajika na vigogo wengine barani Ulaya ikiwa ni pamoja na Galatasaray ya Uturuki na Inter Miami ya Marekani.
Man City haijaonyesha nia ya kuendelea kusalia na Silva kwani haijaanza mazungumzo yoyote licha ya mkataba wake kuelekea kumalizika mwisho wa msimu huu.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, Silva anataka kusubiri hadi itakapomalizika michuano ya Kombe la Dunia inayofanyika Amerika kabla ya kufanya uamuzi wa timu gani atimkie.
Mbali ya timu za Ulaya saini ya Silva pia inahitajika na vigogo wa Saudi Arabia, lakini yeye anaonekana kutamani zaidi kendelea kucheza soka la ushindani barani Ulaya.
Tangu kuanza kwa msimu huu akiwa na Man City amecheza mechi 32 za michuano yote, akifunga mabao mawili na kufanikiwa kutoa pasi tano zilizozalisha mabao.
Julian Brandt
ARSENAL ipo karibu kufanikisha mchakato wa kumsajili kiungo wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Julian Brandt, 29, ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Taarifa zineleza Arsenal imeshafanya hadi makubaliano binafsi na wawakilishi wa Brandt ambaye pia ameahidi kutosaini mkataba mpya ili ajiunge na timu hiyo akiwa mchezaji huru jambo litakalokuwa limeiondolea gharama kubwa Arsenal.
Johan Manzambi
MANCHESTER United, Arsenal na Chelsea zipo katika vita kali ya kuwania saini ya kiungo wa Freiburg na timu ya taifa ya Uswisi, Johan Manzambi mwenye umri wa miaka 20. Manzambi ni miongoni mwa viungo walioonyesha viwango bora katika Ligi Kuu Ujerumani tangu kuanza kwa msimu huu ambapo amecheza mechi 31 za michuano yote na kufunga mabao manne. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika ifikapo 2030.
Sandro Tonali
ARSENAL imeachana na mpango wa kumsajili kiungo wa Newcastle United na timu ya taifa ya Italia, Sandro Tonali, 25. Nyota huyo ambaye ni miongoni mwa mastaa wanaoonyesha viwango bora Ligi Kuu England amekuwa akihitajika na vigogo kibao Ulaya. Kwa mujibu wa taarifa, Tonali anataka kusubiri hadi mwisho wa msimu kuona kama Newcastle itafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya au la kisha ndipo afanya uamuzi.
Nnamdi Collins
LIVERPOOL bado ipo sokoni kutafuta beki mpya itakayemsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi na taarifa zinaeleza rada zimenasa kwa staa wa kimataifa wa Ujerumani anayekipiga Eintracht Frankfurt, Nnamdi Collins, 22. Inaelezwa Liverpool inafuatilia kwa karibu maendeleo ya beki huyo ambaye ameonyesha uwezo mkubwa katika safu ya ulinzi. Hata hivyo, Liverpool haitakuwa peke yake katika mbio za kumsajili Collins kwani Arsenal ipo.
Liam Delap
CHELSEA haina mpango wa kumuuza mshambuliaji wa kimataifa wa England, Liam Delap, 23, katika dirisha lijalo la usajili la majira ya kiangazi. Inaelezwa licha ya Delap kufunga bao moja pekee katika EPL msimu huu ambapo amekuwa nje kutokana na majeraha ya mara kwa mara, viongozi wa Chelsea wana imani kubwa na uwezo wake. Mabingwa hao wa zamani wa England wanaamini mshambuliaji huyo atarejea katika ubora.
Marcus Rashford
BARCELONA imeanza kutazama wachezaji wengine kama mpango mbadala ikiwa haitafanikiwa kufikia makubaliano ya kumsainisha mkataba wa moja kwa moja mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, 28, ambaye anacheza katika kwa mkopo. Rashford kwa sasa anahusishwa na uwezekano wa kuendelea kubaki Camp Nou.
Femi Azeez
CRYSTAL Palace inaongoza katika mbio za kumsajili winga wa Millwall, Femi Azeez, 24, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Inaelezwa Azeez anawindwa na klabu kadhaa za Ligi Kuu England kutokana na kiwango bora alichoonyesha katika michuano ya Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita. Mbali ya Palace, pia anahitajika na Everton na Brentford ambazo zinamfuatilia kwa karibu winga huyo.