Mabondia 50 matajiri zaidi duniani

LONDON, ENGLAND. USHAWAHI kujiuliza, nani ni bondia tajiri zaidi duniani?

Mchezo wa masumbwi ya kulipwa unapata nafasi ya kuzalisha mabondia wenye pesa nyingi kutokana na zile walizovuna kwenye ulingo wa mapambano yao.

Sambamba na hilo, mabondia pia wamekuwa wakinasa dili mbalimbali za matangazo ya kibiashara, ambayo yamekuwa yakiwaimarisha kwenye masuala ya uchumi.

Kutokana na hilo, hii hapa orodha ya mabondia 50 wenye pesa nyingi ambao wanahesabika kuwa matajiri kutokana na vipato vyao wanavyomiliki.


11. Tyson Fury

Utajiri: Dola 65 milioni

Tyson Fury ni bondia Mwingereza na bingwa wa dunia mara mbili kwenye uzito wa juu alipomchapa Deontay Wilder mwaka 2020 na 2021. Staili yake ya upiganaji imemfanya kushinda mapambano mengi na kujiweka kwenye orodha ya mabondia mahiri kabisa kwenye mchezo huo.

Kwa sasa kinachozungumzwa kuhusu Fury ni uwezekano wa kuzipiga na Anthony Joshua, pambano ambalo bila shaka mashabiki wengi wa mchezo huo wanalisubiri kwa hamu. Fury hata mfukoni yupo vizuri, pato lake ni Dola 65 milioni.


10. Vitali Klitschko

Utajiri: Dola 80 milioni

Mwanasiasa wa Ukraine na bondia wa masumbwi ya kulipwa wa zamani, Vitali Klitschko alipigana kwenye masumbwi kati ya ya mwaka 1996 na 2013, ambapo ndani ya muda huo ameshinda mapambano kibao kwenye madaraja tofauti.

Baada ya kustaafu masumbwi, aliamua kuingia kwenye siasa na kuwa meya wa Jiji la Kyiv mwaka 2014.

Vitali alikuwa mmoja wa mabondi wa uzito wa juu moto kabisa na jambo hilo lilimfanya kupata mapambano yenye pesa nyingi na hivyo kuwa miongoni mwa wanamasumbwi matajiri.


9.Anthony Joshua

Utajiri: Dola 80 milioni

Bondia wa masumbwi ya kulipwa Mwingereza, Anthony Joshua alianza mchezo wa ngumi mwaka 2007 na sasa amekuwa mmoja wa mabondia wanaolipwa pesa nyingi duniani.

Alivuna Dola 42 milioni mwaka 2018 na Dola 54 milioni mwaka uliofuata. Bondia Joshua alizungumzia pia pia jinsi anavyoukubali mchezaji wa soka, ambapo mwaka 2012 alifichua timu anayoshabikia kuwa ni Real Madrid na mchezaji anayemhusudu ni Cristiano Ronaldo.

AJ ni miongoni mwa mabondia matajiri, akimiliki Dola 80 milioni.


8.Wladimir Klitschko

Utajiri: Dola 90 milioni

Bondia wa zamani wa masumbwi ya uzito wa juu wa Ukraine, Wladimir Klitschko anatajwa kama mmoja wa mabondia mahiri wa muda wote akipata sifa kutokana na ngumi zake kuwa kali.

Baada ya kutamba kwenye Olimpiki, alihamia kwenye masumbwi ya kulipwa na kushinda ubingwa wa uzito mara mbili akishika rekodi ya kushikilia ubingwa kwa muda mrefu. Alikuwa na uhusiano na mwigizaji mrembo Hayden Panettiere na ana mtoto mmoja wa kike, huku utajiri wake ukitajwa Dola 90 milioni.


7.Sugar Ray Leonard

Utajiri: Dola 120 milioni

Bondia wa zamani wa masumbwi ya kulipwa, Mmarekani Sugar Ray Leonard alitamba kwenye mchezo huo kwa zaidi ya miongo miwili na kushinda mataji kibao ya uzito tofauti.

Sugar Ray alikuwa bondia wa kwanza kuvuna zaidi ya Dola 100 milioni na alishinda tuzo kibao kama za Bondia Bora wa Mwaka na amewekwa kwenye Boxing Hall of Fame. Sugar Ray pia ni mshauri wa filamu mbalimbali ikiwamo ya kisayansi kama ile ya Real Steel iliyochezwa na Hugh Jackman na The Fighter. Ni tajiri.


6. Lennox Lewis

Utajiri: Dola 140 milioni

Bondia Mwingereza Lennox Lewis anatambulika kama mmoja wa wana masumbwi mahiri kabisa kwenye historia ya Uingereza, akipigana mapambano ya kibabe sana dhidi ya wapiga ngumu matata kama Evander Holyfield na Mike Tyson. Lewis alikuwa bingwa wa dunia wa ubingwa wa juu mara tatu na alistaafu baada ya kuzipiga na Vitali Klitschko mwaka 2003.

Nje ya ulingo, Lewis amekuwa akitokea kwenye mambo mbalimbali, ikiwamo kwenye video ya Jennifer Lopez ya wimbo wake All I Have.


5. Saul Alvarez

Utajiri: Dola 180 milioni

Bondia wa ngumi za kulipwa wa Mexico, Saul Alvarez ni moja ya wapiga ngumu matata kabisa kwenye ulingo wa masumbwi duania, akiwa bingwa wa dunia kwenye madaraja manne. Na kinachoelezwa kuhusu bondia huyo kuwa na utajiri unaokadiriwa kuwa Dola 180 milioni.

Akipigana kwenye mapambano ya uzito tofauti, alishinda mapambano 39 kati ya 57 kwa knockout na alipigana na mabondia mahiri kabisa kama Floyd Mayweather na Gennady Golovkin. Alishinda mikanda WBA, WBC akionyesha ubabe.


4. Oscar De La Hoya

Utajiri: Dola 200 milioni

Bondia mstaafu wa ngumi za kulipwa Oscar De La Hoya alianza masumbwi yake 1992 na kupachikwa jina la The Golden Boy kutokana na namna alivyokuwa akishinda mapambano yake ulingoni. Kwa zaidi ya miaka 17 alipigana kwenye masumbwi ya kulipwa na alishinda ubingwa wa dunia mara 11 katika madaraja sita tofauti. Nje ya masumbwi alifanya uwekezaji mkubwa, ikiwamo kwenye taasisi ya huduma za kifedha ya PHP. Bondia huyo anaripotiwa kuwa na pato linalofikia Dola 200 milioni.


3.Manny Pacquiao

Utajiri: Dola 200 milioni

Manny Pacquiao anatajwa kama mmoja wa mabondia mahiri kabisa wa muda wote huku akipata mafanikio katika madaraja nane tofauti na kubeba ubingwa wa dunia.

Ukiweka kando ubondia, Pacquiao ni mwimbaji, mwigizaji na mwanasiasa na ameonekana kwenye filamu nyingi za Kifilipino na alichaguliwa kuwa mbunge kwenye Bunge la Ufilipino mwaka 2010. Utajiri wake unatajwa kuwa Dola 200 milioni, huku Pacquiao akiwa mmoja wa mabondia waliokuwa wakilipwa pesa nyingi, alivuna zaidi ya Dola 1 bilioni.


2.George Foreman

Utajiri: Dola 300 milioni

Bondia wa zamani wa ngumi za kulia na mjasiriamari George Foreman ni mmoja wa watu waliopata utajiri mkubwa kwenye masumbwi. Alishinda medali ya dhahabu ya Olimpiki na ubingwa wa dunia wa uzito wa juu mara mbili.

Lakini, sehemu kubwa ya utajiri wake, Foreman aliupata nje ya mchezo wa masumbwi kupitia kampuni zake mbalimbali.

Ni mshirika pia kwenye timu ya mbio za magari ya Panther Racing Indy, huku akiwa ametunga pia vitabu mbalimbali na amekuwa akicheza filamu pia.


1.Floyd Mayweather

Utajiri: Dola 450 milioni

Mmarekani Floyd Mayweather ndiye bondia tajiri zaidi duniani, akiwa na utajiri unaokisiwa kuwa Dola 450 milioni alizovuna kupitia mapambano yake pamoja na dili za udhamini.

Pambano lake dhidi ya Conor McGregor – lilimpatia pesa nyingi sana. Katika kipindi chake cha ubondia, Mayweather alivuna zaidi ya Dola 1 bilioni na kuwa kwenye jukwaa la wanamichezo waliovuna pesa nyingi kama ilivyo kwa Tiger Woods, Michael Schumacher na Michael Jordan.


Mabondia wengine

50. Dillian Whyte (Dola 7 milioni),

49.Roy Jones Jr (Dola 7 milioni),

48. Kubrat Pulev (Dola 8 milioni),

47.Luis Ortiz (Dola 8 milioni),

46.Terence Crawford (Dola 8 milioni),

45.Daniel Jacobs (Dola 10 milioni),

44.Ryan Garcia (Dola 10 milioni),

43.Timothy Bradley (Dola 10 milioni),

42.Sugar Shane Mosley (Dola 10 milioni),

41.Steve Collins (Dola 10 milioni),

40.Shannon Briggs (Dola 10 milioni),

39.Sergio Martinez (Dola 10 milioni),

38.Regilio Tuur (Dola 10 milioni),

37.Laila Ali (Dola 10 milioni),

36.Julio César Chávez (Dola 10 milioni),

35.Joshua Clottey (Dola 10 milioni),

34.Joe Calzaghe (Dola 10 milioni),

33.Frank Bruno (Dola 10 milioni),

32.Andy Ruiz Jr. (Dola 10 milioni),

31.David Diaz (Dola 15 milioni),

30.Buster Douglas (Dola 15 milioni),

29.Antonio Margarito (Dola 15 milioni),

28.Larry Holmes (Dola 18 milioni),

27.Nigel Benn (Dola 20 milioni),

26.Juan Manuel Marquez (Dola 20 milioni),

25.Freddie Roach (Dola 20 milioni),

24.David Haye (Dola 20 milioni),

23.Carl Froch (Dola 20 milioni),

22.Sonny Bill Williams (Dola 25 milioni),

21.Miguel Cotto (Dola 25 milioni),

20.Gennady Golovkin (Dola 30 milioni),

19.Felix Trinidad (Dola 30 milioni),

18.Deontay Wilder (Dola 30 milioni),

17.Anthony Mundine (Dola 30 milioni),

16.Andre Berto (Dola 30 milioni),

15.Naseem Hamed (Dola 33 milioni),

14.Ricky Hatton (Dola 40 milioni),

13.Bernard Hopkins (Dola 40 milioni),

12.Amir Khan (Dola 40 milioni).