Maandalizi Ligi ya Mabingwa Ulaya, PSG yapata ahueni Ufaransa
Muktasari:
- Mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, wamewasilisha ombi maalum la kuahirishwa kwa mechi ya Ligue 1 dhidi ya FC Nantes ili kuhakikisha kikosi cha kocha Luis Enrique kinakuwa katika hali bora kimwili kuelekea mechi ya mkondo wa pili dhidi ya Chelsea, ugenini.
PARIS Saint-Germain imepata faida muhimu kabla ya mechi ya mkondo wa pili hatua ya 16 bora Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Chelsea itakayochezwa Jumanne, Machi 17, 2026, katika uwanja wa Stamford Bridge kuanzia saa 5:00 usiku kwa muda wa Tanzania.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, wamewasilisha ombi maalum la kuahirishwa kwa mechi ya Ligue 1 dhidi ya FC Nantes ili kuhakikisha kikosi cha kocha Luis Enrique kinakuwa katika hali bora kimwili kuelekea mechi ya mkondo wa pili dhidi ya Chelsea, ugenini.
PSG itakuwa mwenyeji katika mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England katika uwanja wa Parc des Princes Jumatano, Machi 11, 2026, saa 5:00 usiku kwa muda wa Tanzania.
Awali, mabingwa hao wa Ufaransa walipangwa kucheza dhidi ya Nantes mwishoni mwa wiki kati ya michezo hiyo miwili na Chelsea. Hata hivyo, PSG imeomba mechi hiyo ya Ligue 1 kuahirishwa ili kuepusha uchovu wa wachezaji na kutoa nafasi ya maandalizi bora.
Kupitia taarifa rasmi, Ligue de Football Professionnel (LFP) imethibitisha kupokea ombi hilo kutoka PSG, na pia ikaeleza kuwa Nantes imekubali kuahirishwa kwa mechi hiyo.
PSG imefuzu hatua ya 16 bora kupitia mtoano baada ya kuiondosha Monaco kwa jumla ya mabao 5-4 kufuatia kumaliza nje ya nafasi nane za kwanza katika mfumo wa ligi.
Kwa upande wa Chelsea, imefanikiwa kufuzu moja kwa moja baada ya kumaliza katika nafasi nane za juu kwenye mfumo wa ligi. Klabu hiyo ya Ligi Kuu England ilionesha uthabiti katika mechi zake za awali na kuhakikisha inapata alama muhimu zilizoivusha kwenda hatua ya mtoano.
Kwa mujibu wa mfumo mpya wa mashindano hayo, timu nane za juu zilifuzu moja kwa moja kwenda hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku zilizokamata nafasi ya tisa hadi 24 zikacheza mtoano na zilizoshinda zikaungana na zile nane za juu kucheza 16 bora.