Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Luka Modric, Milan wamalizana

MODRIC Pict

Muktasari:

  • Mchezaji huyo wa kimataifa wa Croatia mwenye umri wa miaka 39 tayari ametangaza kuwa ataondoka Madrid ikiwa ni baada ya kuhudumu kwa misimu 13.

MADRID,  HISPANIA: KIUNGO wa Real Madrid, Luka Modric anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya na AC Milan mwezi ujao baada ya Kombe la Dunia la Klabu kumalizika.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Croatia mwenye umri wa miaka 39 tayari ametangaza kuwa ataondoka Madrid ikiwa ni baada ya kuhudumu kwa misimu 13.

Licha ya kutangaza kuondoka, Modric amejumuishwa katika kikosi cha Kombe la Dunia la Klabu chini ya kocha mpya ambaye pia ni mchezaji mwenzake wa zamani, Xabi Alonso.

Kwa mujibu wa ripoti, kiungo huyo amekubali kujiunga na AC Milan mara mkataba wake na Real Madrid utakapomalizika.

Hata hivyo, nyota huyo wa zamani wa Tottenham hataki kufanya uhamisho huo rasmi wala kufanyiwa vipimo vya afya kwa sasa, kwani anataka kuielekeza akili yake katika michuano tajwa hadi pale itakapomalizika ndio aanze na harakati za usajili.

Kikosi cha Alonso kitaanza kampeni yake ya Kombe la Dunia la Klabu kwa kuvaana na Al-Hilal huko Miami Juni, 18. Baada ya hapo, watacheza mechi dhidi ya Pachuca na RB Salzburg kukamilisha hatua ya makundi.

Licha ya timu kutoka Saudi Arabia na Marekani kutaka kumsajili, Modric ameamua kuendelea kucheza soka barani Ulaya.

Gwiji huyo wa Croatia anatamani kuiwakilisha nchi yake kwenye Kombe la Dunia la mwakani, ambapo atakuwa na umri wa miaka 40.

Modric alijiunga na  Madrid kutoka Spurs mwaka 2012 na tangu wakati huo ameichezea Los Blancos mechi 591.

Katika kipindi chake akiwa mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa Madrid, ameshinda taji la  Ligi ya Mabingwa Ulaya mara sita na pia alishinda tuzo ya Ballon d’Or mwaka 2018.

Licha ya kuwa mchezaji mkongwe, Modric alicheza mechi 57 katika michuano yote kwa msimu uliomalizika zikiwemo 35 za La Liga.

Mchezaji huyo mwenye uzoefu alivalia kitambaa cha unahodha mara kadhaa chini ya kocha wa zamani Carlo Ancelotti.

Hata hivyo, Modric ameanza kujiandaa na maisha baada ya soka kwani, Aprili mwaka huu ilithibitishwa kuwa  alinunua sehemu ya hisa za timu ya Swansea City inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza, England.

SunSport iliripoti kuwa Modric alikuwa karibu kununua nyumba ya thamani ya Pauni 1.1 milioni pembezoni mwa jiji la Swansea, Wales.