Liverpool yaendelea kushusha vyuma

Muktasari:
- Mabingwa hao wa Ligi Kuu England wanapanga kutumia kiasi kikubwa tena kwa mshambuliaji mwingine, hata watakapokamilisha dili la usajili wa kuvunja rekodi ya England la kiungo wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL iko mbioni kumsajili nyota wa Paris Saint-Germain, Bradley Barcola ikiwa ni mwendelezo wa kutumia bajeti ya zaidi ya Pauni 300 milioni katika dirisha hili.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu England wanapanga kutumia kiasi kikubwa tena kwa mshambuliaji mwingine, hata watakapokamilisha dili la usajili wa kuvunja rekodi ya England la kiungo wa Bayer Leverkusen, Florian Wirtz.
Taarifa zinaeleza Liverpool iko tayari kushindana na Bayern Munich kwa ajili ya kumsajili winga Barcola, 22, anayekadiriwa kugharimu Pauni 100 milioni.
Mbali ya staa huyo pia Liverpool pia haijakata tamaa kabisa katika mpango wa kumsajili straika wa Newcastle United, Alexander Isak.
Benchi la ufundi la Liverpool linataka mshambuliaji mwingine ambaye ataziba pengo la Darwin Nunez ambaye anaweza kuondoka katika dirisha lijalo.
Hata hivyo, Newcastle inahitaji kiasi kinachoweza kufikia Pauni 150 milioni kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Sweden mwenye umri wa miaka 25.
Barcola ameibuka kuwa mpango mbadala mzuri baada ya kuvutiwa sana na kiwango alichoonyesha katika michuano ya kimataifa akiwa na PSG.
Majogoo hao wa Anfield tayari wametumia Pauni 29.5 milioni kumsajili beki Jeremie Frimpong, 24, kutoka Leverkusen na wako karibu kumsajili beki wa kushoto wa Bornemouth, Milos Kerkez kwa Pauni 40 milioni.
Barcola, ambaye pia ni chaguo la kwanza kwenye orodha ya mastaa wanaohitajika na Bayern, anataka kuondoka ili kutafuta changamoto mpya kwingineko.
Alianzia benchini katika fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter Milan mwezi uliopita, akiingia dakika ya 67 na kutoa pasi ya bao kwa Senny Mayulu katika ushindi wa 5-0.