Liverpool yachapwa Anfield

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Liverpool, England. Majogoo wa jiji Liverpool wamejiweka katika mazingira magumu katika vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England Premier, baada ya kukumbana na kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Crystal Palace.

Baada ya kichapo cha 3-0 nyumbani dhidi ya Atalanta katikati ya wiki katika michuano ya Europa League, wengi walitarajia Crystal Palace itakutana na ghadhabu ya Liverpool lakini haikuwa hivyo.

Jahazi la Liverpool katika mchezo huo, lilizamishwa na Eberechi Eze katika dakika ya 14 tu baada ya pasi nzuri ya mwisho iliyopigwa na Tyrick Mitchell na kuwanyamazisha mashabiki waliokuwa wamejazana Anfield.

Licha ya mabadiliko kadhaa ambayo Liverpool iliyafanya mwanzoni mwa kipindi cha pili kwa kuwatoa Endo, Bradley, Diaz na Nunez huku wakiingia Szoboszlai, Alexander-Arnold, Diogo Jota na Gakpo yalishindwa kuzaa matunda.

Huu ni mchezo wa nane mfululizo Liverpool inaruhusu bao kwenye uwanja wa nyumbani, hali inayoonyesha tatizo kwenye eneo la ulinzi.

Matokeo hayo yameifanya Liverpool kuendelea kusalia katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 71 sawa na Arsenal ambayo ipo uwanjani ikivaana na Aston Villa ili kuishusha Man City iliyopo kileleni na pointi 73.