Liverpool yaanza kumnyemelea Rodrygo kisa mchongo wa Salah

Mabosi wa Liverpool wamepanga kumsajili winga wa Real Madrid, Rodrygo, 22, katika dirisha lijalo la majira ya baridi ikiwa staa wao kutoka Misri, Mohamed Salah, 31, ataamua kuondoka kwenye dirisha hilo.
Salah ambaye alikuwa akiwindwa na Al-Ittihad ya Saudi Arabia tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi anaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuondoka mwakani kutokana na ofa nono aliyowekewa mezani.
Liverpool ina matumaini ya kuvuna kiasi kisichopungua Pauni 200 milioni kwenye mauzo yake na itatumia pesa hiyo kumnyakuwa Rodrygo.
Hata hivyo, inaonekana kuwa ni ngumu sana kwa dili hili la Rodrygo kukamilika kwa sababu ana mkataba hadi mwaka 2025 na kuna kipengele ambacho kinaeleza kwamba ikiwa kuna timu inataka kumnunua itatakiwa kutoa kiasi sichopungua Pauni 900 milioni.
Rodrygo ambaye ana uraia wa Hispania na Brazil ana uwezo wa kucheza maeneo matatu tofauti kwa usahihi ikiwa pamoja na eneo la winga wa kulia, winga wa kushoto na mshambuliaji wa kati.