Liverpool v Arsenal, gemu ya Eze!
Muktasari:
- Timu hizo mbili za makocha Arne Slot na Mikel Arteta zote zimeanza msimu vizuri na kwenye dirisha la usajili kila moja ilitumia pesa za kutosha kuboresha vikosi vyao kuwa vya kiushindani.
Liverpool, England: LIVERPOOL na Arsenal kinapigwa Jumapili ikiwa ni moja ya mechi ya kibabe kabisa ya msimu.
Timu hizo mbili za makocha Arne Slot na Mikel Arteta zote zimeanza msimu vizuri na kwenye dirisha la usajili kila moja ilitumia pesa za kutosha kuboresha vikosi vyao kuwa vya kiushindani.
Liverpool ilianza kwa ushindi wa 4-2 dhidi ya Bournemouth kabla ya kuichapa Newcastle 3-2. Arsenal yenyewe iliichapa 1-0 Manchester United na kisha kuibabua Leeds United 5-0.
Lakini, kipute cha Super Sunday kitakachopigwa Anfield kinatoa taswira ya mbio za ubingwa.
Arsenal imekumbua na majeraha ya wachezaji muhimu, Bukayo Saka na Martin Odegaard, ambaye yupo kwenye hatihati. Hata hivyo, kukosekana kwa Saka, kutatoa nafasi kwa mkali mpya wa Arsenal, aliyesajiliwa kwa Pauni 68 milioni, Eberechi Eze kucheza mechi yake ya kwanza.
Na jambo hilo linampa kocha Slot kasheshe zito la kuanza kufikiria namna ya kumdhibiti Eze.
Liverpool itamzuiaje Eze? Kwa lugha nyepesi, huo ni mtihani mgumu. Eze ni mchezaji mahiri sana hasa mpira unapokuwa kwenye miguu yake na hakika Liverpool itakuwa kwenye wakati mgumu kumdhibiti. Kwa kuangalia mechi ile dhidi ya Newcastle iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani, Arteta anaweza kuwapa wakati mgumu Liverpool kwa kuwakabia kwa juu.
Hilo litampa nafasi Eze kuwaweka kwenye kipindi kigumu mabeki wa Liverpool, endapo kama Arsenal itaweza kupokonya mipira kwenye eneo la juu ya kumpatia mchezaji huyo afanya yake kwenye wingi ya kushoto, huku Noni Madueke akisukuma jambo wingi ya kulia.
Vipi kuhusu Zubimendi? Huo ni usajili mwingine wa Arsenal, ambapo Mhispaniola huyo jukumu lake kubwa litakuwa kuilinda safu ya ulinzi, akicheza kiungo ya kukaba, akimrithi Thomas Partey.
Kwenye mechi ya Leeds alionyesha kiwango bora sana na bila ya shaka Arteta atahitaji tena huduma yake nzuri ili kufanya mambo kuwa mepesi katikati ya uwanja, eneo ambalo Liverpool imekuwa ikijaza wachezaji wengi ili kuwa na umiliki wa mpira.
Je, Florian Wirtz atavuruga mipango ya Arsenal? Kiungo Wirtz tayari ameshaonyesha kwamba ni ingizo muhimu kwenye kikosi cha Liverpool. Lakini, ada iliyolipwa kupata saini yake inawafanya Liverpool kuhitaji mambo makubwa zaidi kutoka kwake, hasa kwenye mechi kubwa na zenye ushindani kama hiyo ya kuwakabili Arsenal, ambao ni wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa.
Wirtz anatarajia kuwa kiungo muhimu kwa washambuliaji wa Liverpool, akiwamo Cody Gakpo, Mohamed Salah na Hugo Ekitike.