Liverpool, Inter Milan vita kali kwa Joshua Kimmich

Muktasari:
- Kimmich mwenye umri wa miaka 30, mkataba wake na Bayern unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa hakuna mwafaka uliofikiwa juu ya kumwongezea muda ili aendelee kubaki.
INTER Milan imejitosa katika vita dhidi ya Liverpool ili kuipata huduma ya kiungo wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani, Joshua Kimmich dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kimmich mwenye umri wa miaka 30, mkataba wake na Bayern unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na hadi sasa hakuna mwafaka uliofikiwa juu ya kumwongezea muda ili aendelee kubaki.
Kiungo huyu alianza kuhusishwa na timu mbalimbali Ulaya tangu mwaka jana, lakini bado ilishindikana kuipata saini yake kutokana na kiasi kikubwa cha pesa kilichohitajika na Bayern.
Tangu kuanza kwa msimu, Kimmich mwenye umri wa miaka 30, amecheza mechi 26 za michuano yote, amefunga bao moja na kutoa asisti 10.
Staa huyu tegemeo wa Bayern kwa sasa yupo nje kutokana na majeraha yanayotarajiwa kumweka nje kwa muda.
Bart Verbruggen
KIPA wa Brighton raia wa Uholanzi, Bart Verbruggen, 22, yupo kwenye rada za Chelsea inayofikiria kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Chelsea inahitaji kumsajili kipa huyu baada ya kiwango kibovu kilichoonyeshwa na makipa wao ambao wamekuwa na makosa mengi tangu kuanza kwa msimu huu. Miamba ya Ligi Kuu ya Ujerumani, Bayern Munich huenda pia ikaingilia kati dili hilo la kunasa saini ya kipa huyo ambaye amekuwa bora.
Adam Wharton
MASKAUTI wa Real Madrid wamekuwa bize kumtazama kiungo wa Crystal Palace raia wa England, Adam Wharton tangu kuanza kwa msimu huu. Wharton mwenye umri wa miaka 21, amekuwa katika rada za vigogo hao baada ya kiwango chake bora alichoonyesha akiwa na timu ya vijana ya England. Nyota huyo pia anawindwa na miamba ya Ligi Kuu England, Liverpool ambayo inaweza ikaondokewa na mastaa wake dirisha lijalo.
Benjamin Sesko
MANCHESTER United, Tottenham na Arsenal zote zimeonyesha shauku ya kuhitaji huduma ya straika wa RB Leipzig na Slovenia, Benjamin Sesko, 22, ambaye katika mkataba wake kuna kipengele kinachomwezesha kuondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa Euro 80 milioni. Ripoti zinadai Leipzig italazimika kumuuza fundi huyu ikiwa itashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Joao Pedro
STRAIKA wa Brighton raia wa Brazil, Joao Pedro, 23, anataka kujiunga na Liverpool katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya timu hiyo kuonyesha nia ya kutaka kumsajili tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Pedro ameivutia sana Liverpool kutokana na kiwango bora alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu na amecheza mechi 23 za michuano yote na kufunga mabao saba.
Jonathan David
MSHAMBULIAJI wa Lille na timu ya taifa ya Canada, Jonathan David amekataa ofa ya kuongeza mkataba mpya wa kusalia timu hiyo na badala yake anataka kuondoka kama mchezaji huru ifikapo mwisho wa msimu. Jonathan ambaye anamaliza mkataba mwisho wa msimu huu anahusishwa na timu mbalimbali za England ambazo ni pamoja na Chelsea, West Ham na Arsenal.
Conor Bradley
LIVERPOOL imeanza mazungumzo na beki wa kulia raia wa Ireland, Conor Bradley kwa ajili ya kumwongeza mkataba mpya utakaomwezesha kuitumikia timu hiyo kwa miaka mitano ijayo. Liverpool inataka kumwongeza mkataba staa huyu kwa sababu anaonekana kama mbadala wa Trent Alexander Arnold.
Leroy Sane
TAARIFA zinaeleza mabosi wa Bayern Munich wapo katika hatua nzuri kwenye mazungumzo yao na wawakilishi wa winga wao Leroy Sane, 29, juu ya mpango wa kumwongeza mkataba mpya utakaomwezesha kusalia kwenye timu hiyo kwa muda mrefu zaidi. Sane ambaye alikuwa akihusishwa kuondoka mwisho wa msimu huu anadaiwa kubadilisha mawazo.