Lisandro Martinez... Hii siyo poa!
Muktasari:
- Wolves iliambulia pointi yake ya tatu msimu huu katika mechi 19 za Ligi Kuu England baada ya sare hiyo ya Old Trafford na hivyo kuigomea Man United nafasi ya kutinga Top Four.
MANCHESTER, ENGLAND: BEKI wa Manchester United, Lisadro Martinez amekuwa na hasira baada ya timu hiyo kufanya uzembe na kutoka sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya timu inayoburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, Wolves.
Wolves iliambulia pointi yake ya tatu msimu huu katika mechi 19 za Ligi Kuu England baada ya sare hiyo ya Old Trafford na hivyo kuigomea Man United nafasi ya kutinga Top Four.
Man United sasa imeangusha pointi tisa kutoka kwenye mechi zake tano za mwisho ilizocheza Old Trafford ndani ya wiki sita. Na mechi hiyo ya Wolves ilikuwa mara ya sita kwa Man United kuongoza 1-0 msimu huu na kisha kushindwa kushinda mechi.
Martinez, ambaye alikuwa nahodha wa Man United katika mechi ya pili mfululizo kutokana na Bruno Fernandes kuwa majeruhi, amesema: “Nimehuzunika sana. Hatuwezi kuja hapa na kutoka sare nyumbani kwenye mechi kama hii. Yatupasa kushinda nyumbani. Wapinzani lazima wataabike, lakini hatukupata pointi tatu. Inakera sana.
“Timu ilijitolea kila kitu. Muda mfupi tu, tuliruhusu bao dakika za mwisho za kipindi cha kwanza, hilo linatokea. Tulistahili, yatupasa kuwajibika. Wolves hawastahili ile nafasi wanayoshika, wana timu imara. Tuliwaheshimu. Sote tumehuzunika, tulitarajia matokeo mazuri. Lazima tukubaliane na hilo na kujiandaa na mchezo mwingine.”
Man United ilikosa huduma ya wachezaji wake wanane wa kikosi cha kwanza, lakini kocha Ruben Amorim hataki kulichukua hilo kama kisingizio kwa sababu iliwachapa Newcastle United kwenye Boxing Day ikiwa haina wachezaji saba.
Amorim, 40, amesema: “Hatukutumia hiki kisingizio dhidi ya Newcastle. Hatuwezi kukitumia pia kwenye mechi hii, ukiangalia mchezo utaona kwanini tumecheza tulivyocheza, hatukuwa kwenye ubora wetu na tulipoteza mara nyingi kwenye matukio ya ana kwa ana.”
Baada ya kuachana na fomesheni ya 3-4-2-1 kwenye mechi ya Newcastle na kucheza 4-2-3-1, Amorim alirudi tena kwenye mtindo wake wa mabeki watatu dhidi ya Wolves.
Alipoulizwa kuhusu kurudi tena kwenye 3-4-2-1, Amorim amesema: “Tulijua watacheza na watu watano kati. Watatumia mawinga na wamefanya hivyo.”