Lionel Messi amkataa Jude Bellingham

Messi Pict
Messi Pict

Muktasari:

  • Messi ndiye mchezaji anayeongoza kwa kushinda tuzo hiyo (mara nane) ya mwisho ikiwa ni mwaka jana baada ya kuisaidia Argentina kushinda Kombe la Dunia 2022.

MIAMI, MAREKANI: STAA wa Inter Miami na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi amekataa kulitaja jina la staa wa Real Madrid,  Jude Bellingham katika orodha ya mastaa wanaoweza kushinda tuzo za Ballon d’Or mwaka huu.

Messi ndiye mchezaji anayeongoza kwa kushinda tuzo hiyo (mara nane) ya mwisho ikiwa ni mwaka jana baada ya kuisaidia Argentina kushinda Kombe la Dunia 2022.

Tuzo za mwaka huu zinaonekana huenda zikazalisha mshindi tofauti baada ya Messi na Cristiano Ronaldo kupokezana kwa miaka 15 iliyopita huku Ronaldo akishinda mara tano.

Kwa sasa Ronaldo ambaye yupo zake Saudi Arabia na Messi anayekipiga kule Marekani hawaonekani kuwa na nafasi ya kushinda tuzo hii na vijana wanaofanya vizuri barani Ulaya ndio wanapewa nafasi hiyo.

Miongoni mwa wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda ni staa wa England Jude Bellingham ambaye msimu uliopita alifanya vizuri akiwa na Real Madrid na alifunga mabao 23 katika mechi 42 za michuano yote akisaidia wababe hao kushinda taji la Ligi ya Mabingwa na La Liga.

Mbali ya Jude, mastaa wengine kama Vinicius Jr na Toni Kroos ambao walikuwa na msimu bora ndani ya Madrid, pia Kylian Mbappe yumo.

Bellingham ataongeza uwezekano zaidi wa kushinda tuzo hii ikiwa ataisaidia England kushinda taji la Euro na leo atakuwa na kazi dhidi ya Uholanzi katika mchezo wa hatua ya nusu fainali.

Messi alipowahi kuulizwa juu ya nani anaweza kuchukua tuzo hii kwa mwaka huu hakumjumuisha kabisa Jude.

“Erling Haaland, Kylian Mbappe na Vinicius ni miongoni mwa wachezaji vijana wanaoweza kushinda tuzo hii kwa miaka ijayo, nafikiri pia  Lamine Yamal, ambaye bado ni kijana anaweza akawa mmoja kati ya mastaa wanaoweza kushinda tuzo hii,”  alisema Messi mara baada ya kushinda tuzo mwaka jana.