Lewandowski mbioni kustaafu

Muktasari:
- Lewandowski ambaye alijiunga na Barca akitokea Bayern Munich mwaka 2022, amekuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo wa timu hiyo na msimu huu amefunga mabao 19 katika michezo 17 ya mashindano yote akiiwezesha Barca kukaa kileleni mwa La Liga kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya Real Madrid.
BARCELONA, HISPANIA: MSHAMBULIAJI wa Barcelona, Robert Lewandowski, ameweka wazi kwamba yupo mbioni kuachana na soka licha ya kuwa katika kiwango bora tangu ajiunge na Barcelona.
Lewandowski ambaye alijiunga na Barca akitokea Bayern Munich mwaka 2022, amekuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo wa timu hiyo na msimu huu amefunga mabao 19 katika michezo 17 ya mashindano yote akiiwezesha Barca kukaa kileleni mwa La Liga kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya Real Madrid.
Hata hivyo, mshambuliaji huyu mwenye uzoefu alipofanya mahojiano na tovuti ya Forbes, alisema: “Kwa umri wangu sasa, najua kuwa hivi karibuni naweza kustaafu, inaweza kuwa ni baada ya miaka miwili, mitatu mpira wangu utakuwa umefikia mwisho.”
Ingawa mkataba wake na Barcelona unamalizika mwaka 2026, na kuna chaguo la kuongeza mkataba wa mwaka mmoja, Lewandowski alisisitiza kuwa atastaafu ikiwa atahisi kiwango chake kimekwisha.
“Nitajitathmini mwenyewe na kujiambia ni lini nitamaliza, siku nitakapoamka asubuhi na kujihisi sitaki kwenda kwenye mazoezi, huo utakuwa ni mwanzo wa kufikiria kuhusu kustaafu.”
Hata hivyo, kwa sasa fundi huyu amesema hajihisi kama amechoka na bado ana njaa ya kutaka kuendelea kwani kila siku anapoamka anajisikia hali ya kutaka kwenda mazoezini.
“Nina matumaini itandelea kuwa hivi, bado moyo wangu unapenda kwenda mazoezi wala sihisi maumivu yoyote.”
Barcelona imekuwa ikihusishwa na washambuliaji mbalimbali wanaotajwa kuwa huenda wakachukua nafasi ya staa huyu pale atakapoamua kustaafu na miongoni mwa wanaotajwa ni Victor Gyokeres na Erling Haaland.
“Nadhani ni vigumu kupata mshambuliaji kama Robert leo hii. Kuna mmoja au wawili tu wanaoweza kukupa kiwango kama chake. Labda Haaland, kwa upande wa Gyokeres ni mchezaji mzuri na amekuwa akifunga mabao lakini sio kipaumbele chetu,” alisema mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo, Deco, alipofanya mahojiano na Mundo Deportivo.
Tangu alipoanza kucheza soka la kulipwa akiwa na Znik Pruszkow ya huko Poland, staa huyu amefunga mabao 688 kwa upande wa klabu na timu ya taifa.